Friday 1 August 2008

BAADA YA KUTOLEWA JELA SASA FA YAMSHITAKI BARTON!
Chama cha Soka Uingereza FA kimemtaka mchezaji wa Newcastle Joey Barton, ambae juzi tu alitolewa jela baada ya kutumikia adhabu ya kifungo cha miezi 6 baada ya kumjeruhi kijana mmoja nje ya hoteli mjini Liverpool, ajitetee kwanini hatua za nidhamu zisichukuliwe dhidi yake kwa kumshambulia na kumjeruhi mchezaji mwenzake mazoezini wakati alipokuwa akichezea Timu ya Manchester City.
Tukio hilo la Joey Barton kumpiga na kumuumiza mchezaji mwenzake Mfaransa Ousmane Dabo [pichani ni Ousmane Dabo na Joey Barton] lilitokea mwezi Mei 2007 na lilifikishwa Mahakamani tarehe 1 Julai 2008 ambako alihukumiwa kifungo cha nje cha miezi minne baada ya kukiri kosa.
Hukumu hii ilitoka wakati tayari Barton alikuwa jela akitumia kifungo chake cha miezi 6 kwa kujeruhi.
Endapo atapatikana na hatia basi FA inaweza kumfungia kwa muda mrefu na kumpiga faini.
Klabu ya Newcastle imelalamikia hatua hii ya FA na kuhoji uhalali wa wao kuadhibiwa kwa kosa lililotendeka wakati mchezaji anamilikiwa na klabu jingine. Wakati Barton anatenda kosa hilo alikuwa ni mchezaji wa Manchester City na mfarakano huo ndio uliomfanya ahamishiwe Newcastle. Vilevile, Newcastle imelalamika kwa nini Barton ashitakiwe takriban miezi 15 baada ya kosa lenyewe kutendeka.

No comments:

Powered By Blogger