Monday, 28 September 2009

Arsenal yapata pigo! Kiungo Denilson nje miezi miwili! Klabu ya Arsenal leo imethibitisha kwamba Kiungo wao Mbrazil, Denilson, hataonekana uwanjani kwa miezi miwili baada ya kuvunjika mfupa mgongoni na inasemekana alipata maumivu hayo katika mechi ya tarehe 12 Septemba 2009 Arsenal ilipofungwa 4-2 na Manchester City.
Vile vile imejulikana leo kuwa Mshambuiaji wao kutoka Denmark Nicklas Bendtner hatacheza mechi ya kesho ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE dhidi ya Olympiakos baada ya kupata ajali ya gari ingawa hamna taarifa zaidi zilizopatikana kuhusu janga hilo.
Cech ahoji Kadi Nyekundu aliyotwangwa!!!
Kipa wa Chelsea, Petr Cech, ambae alipewa Kadi Nyekundu na Refa Phil Dowd kwenye mechi ya Ligi Kuu Jumamosi walipofungwa na Wigan 3-1 baada ya kumwangusha Mshambuliaji Hugo Rodallega, amehoji uhalali wa Kadi hiyo kwa kudai kuwa yeye hakuwa mtu wa mwisho kwani Beki wake Ashley Cole alishakuwa nyuma yake kudhibiti shambulizi hilo.
Kwa Kadi hiyo, Cech ataikosa “Ze Bigi Mechi” ya Jumamosi wakati Chelsea watakapowakaribisha Liverpool Stamford Bridge kwenye Ligi Kuu.
Steve Bruce amfokea Straika wake Bent kwa kuikacha Penalti!!!
Meneja wa Sunderland Steve Bruce amekerwa na kitendo cha Mshambuliaji wake Darren Bent kutopiga penalti na kumwachia Mshambuliaji mwenzake Kenwyne Jones kuipiga na kufunga bao la pili la Sunderland katika mechi ambayo Sunderland waliifunga Wolverhampton mabao 5-2 kwenye Ligi Kuu.
Katika mechi hiyo Sunderland walifunga bao la kwanza kwa penalti Mfungaji akiwa Darren Bent ambae Steve Bruce amemtaja kuwa ndie pekee mwenye majukumu ya kupiga penalti za Sunderland.
Mara baada ya mapumziko, huku Sunderland wakiwa 1-0 mbele, Sunderland wakapewa penalty baada ya Darren Bent kuangushwa kwenye boksi na ndipo Kenwyne Jones akamwomba Bent kupiga mkwaju huo na Bent akamwachia Jones aliefunga bao la pili.
Steve Bruce amesema: “Darren Bent ni mpigaji penalti bora duniani na yeye pekee ndie anatakiwa kupiga penalti zetu! Penalti ile ya pili ni muhimu, sasa je tungeikosa wakati tuna bao moja tu? Afadhali ingekuwa tuko mbele 5-0! Ntahakikisha kitendo hiki hakirudiwi!”

No comments:

Powered By Blogger