Apoel Nicosia v Chelsea
Leo saa 3 dakika 45 usiku, saa za bongo, Chelsea wanashuka Uwanja wa GSP Nicosia uliopo mjini Nicosia, Visiwani Cyprus, kucheza na Wenyeji wao Apoel Nicosia katika mechi ya pili Kundini mwao katika kinyang’anyiro cha UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
Chelsea watashuka dimbani bila Nyota wao Michael Ballack, John Mikel Obi na Ashley Cole ambao ni majeruhi pamoja na Didier Drogba na Jose Bosingwa ambao bado wako kifungoni.
Ingawa Apoel Nicosia hawapewi nafasi kubwa kwenye mechi hii, Kocha wao Ivan Jovanovic anaamini wanaweza kufanya vizuri hasa baada ya kucheza vizuri katika mechi ya kwanza walipokuwa ugenini huko Spain na kutoka suluhu na Atletico Madrid.
Chelsea waliifunga FC Porto ya Ureno bao 1-0 katika mechi ya awali ya Kundi hili.
Mechi nyingine kwenye Kundi hili ni FC Porto v Atletico Madrid.
Manchester United v VfB Wolfsburg
Ndani ya Old Trafforf jijini Manchester, Mashetani Wekundu Man U watakwaana na Mabingwa wa Ujerumani Wolfsburg katika mechi ya pili ya Kundi lao kuwania Kombe la UEFA Champions LEAGUE.
Mechi nyingine ya leo kwenye Kundi hili ni kati ya CSKA Moscow v Besiktas.
Man U ilishinda mechi yake ya kwanza Kundini kwa ushindi wa ugenini wa 1-0 dhidi ya Besiktas na Wolfsburg, ikiwa nyumbani, iliibamiza CSKA Moscow 3-1.
Man U leo huenda ikaikosa nguvu kazi ya Winga Park Ji-sung ambae ni mgonjwa na pia upo wasiwasi kuhusu Michael Owen ambae ana tatizo dogo pajani.
Kipa Veterani Edwin van der Sar ameshapona na ameanza mazoezi lakini inaaminika leo Ben Foster ataendelea kuwa golini kwani van der Sar hajapata mazoezi ya kutosha.
Wolfsburg huenda wakamkosa Nahodha wao Josue mwenye matatizo ya goti ambalo alifanyiwa operesheni hivi karibuni.
Hata hivyo, nguvu ya Wolfsburg ni Mshambuliaji hatari toka Brazil Grafite na mwingine kutoka Bosnia, Edin Dzeko, Wachezaji ambao hupewa sapoti kubwa na mwenzao kutoka Bosnia pia aitwae Zvjezdan Misimovic.
No comments:
Post a Comment