Tuesday 29 September 2009

Daktari Mkuu FIFA ataka Marefa kutoa Kadi Nyekundu nyingi!!!
Daktari Mkuu wa FIFA, Michel D’Hooghe, amewataka Marefa wawe wakali zaidi na kutoa Kadi Nyekundu zaidi ili kudhibiti rafu mbaya ambazo huleta madhara makubwa kwa Wachezaji.
Daktari huyo katika utafiti wake amegundua kuwa kutokana na ongezeko la utajiri kwenye Soka vilevile rafu mbaya na kuumia vibaya kwa Wachezaji kumeongezeka kwani utajiri huo umeleta ushindani mkubwa na hivyo Timu na hasa Wachezaji wako tayari kujitoa muhanga ili kupata ushindi kwa njia yeyote ile.
Daktari D’Hooghe anasema: “Refa ndio ufunguo! Yeye akitoa Kadi Nyekundu anahakikisha Mchezaji anaadhibiwa palepale! Hilo litakuwa tishio kwa wengine!”
Utafiti wa Daktari D’Hooghe umeonyesha kuwa katika Fainali za Kombe la Dunia huko Korea na Japan mwaka 2002 Wachezaji 12 waliumia vibaya kwa kupigwa ngwala toka nyuma na vipepsi lakini katika Fainali za Kombe hilo huko Ujerumani mwaka 2006, baada ya Marefa kuagizwa kutoa Kadi Nyekundu bila woga kwa rafu hizo, ni Wachezaji wawili tu ndio waliumizwa.
FIFA U-20 WORLD CUP EGYPT 2009:
Wenyeji Misri watunguliwa dakika za majeruhi!!
Misri 1 Paraguay 2
Misri, ambao ndio wenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia la Vijana wa Chini ya Miaka 20, jana walifungwa na Paraguay mabao 2-1 na goli la ushindi la Paraguay iliyocheza na watu 10 baada ya Mchezaji wao Robert Huth kutolewa kipindi cha kwanza lilifungwa kwenye dakika ya 4 ya dakika za majeruhi.
Kwenye Kundi hili la Misri, Italy na Paraguay ndio wanaoongoza kwa kuwa na pointi 4 kila mmoja na Misri anafuatia akiwa na pointi 3 huku Trinidad & Tobago yuko mkiani bila pointi.
Mechi za mwisho Kundi hili ni Misri v Italy na Paraguay v Trinidad & Tobago.

No comments:

Powered By Blogger