Sunday 27 September 2009

Kufuatia kipigo cha jana, Ancellotti ataka Chelsea ikaze buti!!!!
Bosi wa Chelsea Carlo Ancellotti amekitaka Kikosi chake cha Chelsea kuibuka upya kufuatia kipigo cha 3-1 mikononi mwa Wigan kwenye Ligi Kuu hapo jana na kushinda mechi ya Jumatano watakapocheza UEFA CHAMPIONS LEAGUE na Apoel Nicosia ya Cyprus huko Cyprus.
Mbali ya kipigo hicho, Kipa wa Chelsea Petr Cech alitolewa nje kwa Kadi Nyekundu baada ya kumchezea rafu fowadi wa Wigan Hugo Rodagella na kusababisha penalti iliyopigwa na Rodagella aliefunga na kuipa Wigan bao la pili.
Sasa Cech ataikosa ‘Bigi Mechi’ Jumapili ijayo Chelsea watakapovaana na Liverpool.
Ancellotti alikiri kupandwa na ghadhabu na kuzungumza Kitaliano na Wachezaji lakini alikubali pia Wigan walistahili kushinda kwa kuutumia uwanja wote vizuri.
Kocha wa Stoke akiri wamefungwa na Timu Bora!!!
Meneja wa Stoke City, Tony Pulis, ambae timu yake ilipigwa 2-0 na Manchester United hapo jana kwenye Ligi Kuu uwanjani kwake Britannia, amekubali kuwa walizidiwa kila kitu na timu bora.
Pulis alisema: “Ili kushindana na timu kama Man U, unahitaji kila Mchezaji wako acheze kwa nguvu zote na kiwango cha juu kabisa! Hatukufanya hivyo! Pia, wana Wachezaji wazuri na wazoefu sana kama Giggs na Scholes! Huna cha kufanya bali kuwaheshimu na kuwahusudu tu!!”
Nae Sir Alex Ferguson alizungumza kwa kusema safari bado ni ndefu ingawa kwa sasa wako kileleni.
Benitez ammwagia sifa Torres!!
Fernando Torres, baada ya kupachika mabao matatu katika ushindi wa mabao 6-1 wa Liverpool walipoikung’uta Hull City jana kwenye Ligi Kuu uwanjani Anfield, amemwagiwa sifa kemkem na Meneja wake, Mhispania mwenzake, Rafa Benitez.
Benitez amesema: “Tulimnunua kwa Pauni Milioni 20 na hilo ni dau kubwa kwetu lakini sasa anaonyesha thamani yake! Tuna imani atazidi kuboreka!”
Na, Bosi wa Hull City Phil Brown, ameeleza kukerwa kwake kwa jinsi timu yake ilipoipa Liverpool zawadi ya magoli. Brown amesema: “Watu watasema Torres ndie aliewapa ushindi lakini ukweli ni kwamba tumewapa zawadi ya magoli kwa udhaifu wetu kujihami!”
Ronaldo ni shabiki wa Man U!!! Huganda kwenye TV wakicheza, hushangilia wakishinda!!!
Cristiano Ronaldo, ingawa kwa sasa ni Mchezaji wa Real Madrid baada ya kuihama Manchester United, ameungama kuwa yeye ni Shabiki mkubwa wa Mashetani hao Wekundu!
Ronaldo amesema: “Natizama mechi zao zote! Ingawa nipo Real, nafurahi sana wakishinda!”
Vilevile ameelezea furaha yake kumwona rafiki yake na Mreno mwenzake, Nani, akipata namba mara kwa mara na amekiri kuongea na Nani kwa simu mara kwa mara.
Ronaldo ameeleza: “Nani ni mchezaji mzuri sana na sasa atapata nafasi ya kupanda chati!”
UEFA yachunguza Klabu za Ulaya Mashariki kucheza ‘fiksi!’
UEFA imetangaza kuwa ipo kwenye uchunguzi wa kesi 40 za upangaji matokeo kwenye mechi za UEFA CHAMPIONS LEAGUE na Kombe la UEFA kwa kipindi cha miaka minne iliyopita inayohusisha Klabu za Nchi za Ulaya Mashariki na kati ya hizo mechi 15 ni za katika miaka miwili iliyopita.
Peter Limacher, Mkuu wa Kitengo cha Nidhamu cha UEFA, amesema: “Ni Klabu za Ulaya Mashariki. Wakijua wameshatoka kwenye mashindano, huamua sasa tupate faida na wanapanga matokeo! Uchunguzi utachukua muda lakini tunao ushirikiano wa Polisi.”
Mwezi uliokwisha UEFA ilitangaza inachunguza Klabu 3 za Macedonia baada ya kuwafungia Mabingwa wa Nchi hiyo Klabu ya FK Pobeda kutoshiriki michezo ya Ulaya kwa miaka minane.
Moja ya mechi zinazochunguzwa ni ile ya Klabu ya Macedonia FK Milano ilipokung’utwa jumla ya mabao 12-2 katika mechi 2 walipotolewa na Klabu ya Croatia Slaven Koprivnica katika Raundi ya Pili ya EUROPA LIGI mwezi Julai mwaka huu.

No comments:

Powered By Blogger