Saturday 3 October 2009

Fergie na Torres ni Bora Septemba
Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, na Straika wa Liverpool, Fernando Torres, wameshinda Tuzo ya Ligi Kuu England ya Meneja Bora na Mchezaji Bora kwa mwezi Septemba.
Sir Alex Ferguson ameshinda Tuzo ya Meneja Bora ikiwa ni mara yake ya 24 kuitwaa kwa kuiongoza Manchester United kushika uongozi kwenye Ligi Kuu baada ya kushinda mechi zao zote za mwezi Septemba ambapo walianza kwa kuifunga Tottenham huko White Hart Lane 3-1, kisha kuwafunga Watani wao Man City 4-3 Old Trafford na kushinda Britannia Stadium 2-0 dhidi ya Stoke City.
Man U vilevile walicheza mechi mbili za UEFA CHAMPIONS LEAGUE mwezi Septemba na kuifunga Besiktas 1-0 ugenini huko Ugiriki na pia kuilaza Wolfsburg Old Trafford 2-1.
Fernando Torres ametunukiwa Tuzo ya Mchezaji Bora ikiwa ni mara yake ya pili kuipata kwa kufunga mabao matano mwezi Septemba. Torres, mpaka sasa, ndie anaeongoza kwa Ufungaji Bora kwenye Ligi Kuu akiwa na bao 8.
Berbatov aliwahi kutekwa nyara!!!
Mshabuliaji wa Manchester United, Dimitar Berbatov, ametoboa kuwa miaka 10 iliyopita alitekwa nyara na Gangsta mkubwa huko kwao Bulgaria aitwae Georgi Iliev aliewatuma vibaraka wake watatu kumkamata ili kumlazimisha asaini Klabu ya Levski Kjustendil iliyomilikiwa na jambazi hilo.
Wakati huo, Berbatov alikuwa Mchezaji wa CSKA Sofia huko Bulgaria.
“Ni kweli!” Berbatov alithibitisha. “Ilitisha lakini nilifanikiwa kumpigia simu Baba yangu alieniokoa!”
Akizungumzia presha anayoipata kwa kuchezea Klabu kubwa kama Manchester United, Berbatov alisema: “Ni presha kubwa! Sibishi kuwa mtu akilipa pesa nyingi kwa ajili yako anategemea vitu vikubwa toka kwako!”
Kesho ni “Ze Bi Mechi” huko Scotland: Rangers v Celtic!!!
Ingawa Timu hizo vigogo za Scotland hazifanyi vizuri kwenye mashindano ya UEFA huko Ulaya huku Rangers wakiwa mkiani kwenye Kundi lao la UEFA CHAMPIONS LEAGUE na Celtic wakiwa mkiani pia Kundini mwao kwenye EUROPA LIGI, kesho Uwanja wa Ibrox, nyumbani kwa Rangers, moto utawaka kwenye “dabi” inayozikutanisha Timu za Glasgow huko Scotland.
Mpaka sasa Celtic yuko mbele ya Rangers kwa pointi 4 baada ya mechi 6 na ndie anaeongoza Ligi Kuu Scotland akiwa na pointi 16.
Rangers ndie Bingwa Mtetezi wa Scotland.

No comments:

Powered By Blogger