Monday 28 September 2009

LEO MAN CITY v WEST HAM!!!!
Gianfranco Zola: "Bellamy alinifanya niwe Meneja Bora!!"
Meneja wa West Ham ambae aliwahi kuwa Staa wa Chelsea, Gianfranco Zola, amepasua kuwa Mchezaji mkorofi sana Craig Bellamy ambae sasa yuko Manchester City alimpa wakati mgumu alipokuwa West Ham na kumfanya yeye aongezeke uzoefu wa kuwa Meneja Bora.
Bellamy, Raia wa Wales, aliihama West Ham Januari mwaka huu na kujiunga na Manchester City.
Bellamy alipokuwa Liverpool ilibidi aihame Timu hiyo baada ya kudaiwa kumpiga na gongo la kuchezea Gofu mchezaji mwenzake John Riise na ashawahi kufarakana na Alan Shearer alipokuwa Newcastle.
Wiki moja iliyopita Bellamy alitawala vichwa vya habari Magazetini baada ya kumzaba kibao shabiki alievamia Uwanja wa Old Trafford baada ya mechi kati ya Man U na Man City kumalizika kwa ushindi wa 4-3 kwa Man U.
FA, Chama cha Soka cha England, kimempa onyo kali Bellamy kwa kitendo hicho.
Na leo usiku, Timu ya Craig Bellamy, Manchester City, itapambana na Klabu yake ya zamani, West Ham na Meneja wa West Ham, Gianfranco Zola ametamka: "Nilipenda kufanya nae kazi! Ni kitu kigumu kwani ni mtu mwenye munkari! Lakini ukimchukulia kwa njia ipasayo ni Mchezaji anaekulipa kwa juhudi zake uwanjani!"
Zola ameendelea: "Amenipa uzoefu na manufaa katika kazi ya Umeneja!"
John Terry awakandya wenzake Chelsea!!
Nahodha wa Chelsea, John Terry, amewalaumu sana Wachezaji wenzake kufuatia kipigo chao cha Jumamosi cha mabao 3-1 walichoangushiwa na Timu 'dhaifu' Wigan ambayo katika mechi zake mbili za nyuma ilibugizwa 5-0 na Manchester United na 4-0 na Arsenal.
Kipigo hicho toka kwa Wigan na ushindi wa Man U wa bao 2-0 dhidi ya Stoke City kumewafanya Man U ambao ndio Mabingwa Watetezi, kushika hatamu LIGI KUU England.
Chelsea, ambao hawajachukua Ubingwa kwa miaka mitatu sasa tangu wautwae kwa mara mbili mfululizo chini ya Meneja Jose Mourinho, inaelekea wamekerwa sana na kipigo hicho na kufikia hatua ya kumfanya Terry kudiriki kuanika mzozo wao wa ndani ya Klabu hadharani.
Terry amekaririwa akilalama: "Ni kawaida kucheza vibaya lakini hata ukicheza vibaya unategemea Wachezaji wenzako kujituma na kupigana! Timu nzima haikufanya hivyo! Timu kubwa zote zimeshinda wikiendi hii na hili linavunja moyo! Tuna mechi Jumatano, itabidi tufanye vizuri! Na Jumapili ijayo tuna mechi ngumu na Liverpool na itabidi tujitutumue!" 

No comments:

Powered By Blogger