Leo Arsenal v Olympiakos na Fiorentina v Liverpool
Arsenal watajimwaga nyumbani Emirates Stadium kuwakaribisha Olympiakos na Liverpool watakuwa Nchini Italia kupambana na Fiorentina zikiwa ni mechi za pili kwa kila Timu katika Makundi yao.
Arsenal alifungua dimba huko Ubelgiji na kuibwaga Standard Liege mabao 3-2 wakati Liverpool alianza kampeni zake nyumbani Anfield na kuwafunga Debrecen bao 1-0.
Leo Arsenal watacheza bila ya Kipa nambari wani Manuel Almunia ambae ni mgonjwa na nafasi yake itachukuliwa na Kipa mdogo toka Italia Vito Mannone ambae aling’ara kwenye mechi ya Ligi Kuu Arsenal aliyoifunga Fulham bao 1-0 hapo juzi.
Arsenal pia itawakosa Kiungo Denilson ambae ameumia na atakuwa nje ya uwanja kwa miezi miwili pamoja na Mshambuliaji Nicklas Bendtner aliepata ajali ya gari siku ya Jumapili.
Hata hivyo Arsenal wana habari njema kwamba huenda Chipukizi Nyota Theo Walcott ambae hajacheza tangu Juni kwa kuwa na maumivu huenda akawepo leo.
Olympiakos, ambao wana Kocha mpya Nyota wa zamani wa Brazil Zico alieanza kazi hiyo Septemba 17, walianza kampeni yao kwenye Kombe hili kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AZ Alkmaar.
Liverpool watapambana huko Italia na Fiorentina klabu ambayo ilipoteza mechi yake ya kwanza kwenye mashindano haya walipofungwa bao 1-0 na Lyon na pia Mshambuliaji wao nyota Alberto Gilardino kutolewa kwa Kadi Nyekundu baada ya kumpiga kipepsi Jeremy Toulalan wa Lyon katika mechi hiyo.
Kukosekana kwa Gilardino kutatoa nafasi kwa Mshambuliaji wa zamani wa Chelsea Adrian Mutu na mwenziwe Stevan Jovetic kuanza mechi hii.
Liverpool watakuwa na pengo kwani itawakosa Viungo Javier Mascherano na Yossi Benayoun ambao ni majeruhi na pengo hilo huenda likazibwa na Albert Riera.
No comments:
Post a Comment