Thursday 5 November 2009

Benni McCarthy kuhama Blackburn Januari ili apate namba!!
Mshambuliaji toka Bondeni, Benni McCarthy, ambae kwa sasa anapigwa benchi na Timu yake Blackburn Rovers anataka kuihama Timu hiyo ili aende kwingine ambapo atapata namba na hivyo kupata nafasi kubwa ya kuchukuliwa Kikosi cha Timu ya Taifa ya Afrika Kusini kitakachocheza Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika huko huko kwao kuanzia Juni 11, 2010 hadi Julai 11, 2010.
Habari hizi za kuhama zimethibitishwa na Meneja wa Blackburn Sam Alladyce ambae amesema: “Namwelewa nia yake ni kutaka kucheza kila siku. Lakini kwa sasa hapati namba kwa vile David Dunn amepona na amerudi kwenye fomu. Ikitokea ofa nzuri kwa Benni ntaruhusu ahame!”
Tangu msimu huu uanze, Benni McCarthy ameanza mechi moja tu na ni ile ya ufunguzi Blackburn na Manchester City na mechi nyingine zote amecheza akitokea benchi.
MAN CITY kwenda Abu Dhabi kwa Tajiri wao!!
Mmiliki wa Manchester City Sheikh Mansour bin Zayed Al Nahyan anategemewa kuiona Timu yake ikicheza kwa mara ya kwanza tangu alipoinunua kwa Pauni Milioni 210 Septemba mwaka jana wakati itakapozuru Abu Dhabi na kucheza na Timu ya Taifa ya Falme za Nchi za Kiarabu, UAE, Novemba 12.
Mark Hughes, Meneja wa Man City, anatagemewa kuongoza Kikosi pungufu kwa vile Wachezaji wao Nyota wengi watakuwa kwenye Timu zao za Taifa ambazo zitakuwa kwenye mechi za mwisho za kuwania kuingia Fainali Kombe la Dunia.
Kikosi hicho kitaruka kwenda Abu Dhabi Jumatatu ijayo.
Wiki ya kuanzia Jumatatu hiyo ni wiki ya Timu za Taifa kufuatana na Kalenda ya FIFA.
Sheikh Mansour ni mmoja wa Koo ya Kifalme huko UAE na mwakilishi wake hapo Man City ambae amemteua Mwenyekiti ni Khaldoon al-Mubarak.

No comments:

Powered By Blogger