Monday 2 November 2009

Carragher: “Inauma!!!”
Jamie Carragher amekiri kuwa Liverpool wanaumia sana kwa vipigo mfululizo lakini amewataka Wachezaji wenzake wasife moyo.
Carragher Jumamosi alipewa Kadi Nyekundu katika kipigo cha bao 3-1 walichopewa na Fulham kwenye Ligi Kuu na kuwafanya wawe wamefungwa mechi 6 katika 7 walizocheza mwisho.
Liverpool sasa wako pointi 9 nyuma ya vinara Chelsea na pointi 7 nyuma ya Mahasimu wao Manchester United ambao wako nafasi ya pili.
Mbali ya kuwa nafasi mbaya kwenye Ligi na kupokea vipigo vitano kati mechi 11 za Ligi walizocheza, Liverpool Jumatano iliyopita walibwagwa nje ya Kombe la Ligi baada ya kufungwa 2-1 na Arsenal na hali hii imemfanya Meneja wao Rafa Benitez kukalia kuti kavu.
Jumatano hii Liverpool wana kibarua kikubwa huko Ufaransa watakapokutana na Lyon kwenye UEFA CHAMPIONS LEAGUE, timu ambayo iliifunga Liverpool 2-1 nyumbani kwake Anfield.
Kipigo kingine toka kwa Lyon kutaifanya Liverpool iwe nje ya Kombe hilo la Ulaya na pengine kuwa ndio msumari wa mwisho kwa Benitez.
Faraja pekee kwa Liverpool ni ule ushindi wa 2-0 walioupata baada ya kuwafunga Manchester United lakini hilo pia halimpi moyo Jamie Carragher ambae amesema: “Ni wakati mgumu kwetu na tunaumia sana! Tuliibuka tulipoifunga Man U lakini sasa tumepigwa mechi 2 mfululizo!! Ni sisi Wachezaji pekee ndio tunaweza kuibadili hali hii!”

No comments:

Powered By Blogger