Tuesday 3 November 2009

LEO UEFA CHAMPIONS LEAGUE: Tathmini ya Mechi
RATIBA: Jumanne, 3 Novemba 2009
[saa 4 dak 45 usiku]
KUNDI A
Bayern Munich v Bordeaux,
Maccabi Haifa v Juventus,
KUNDI B
Manchester United v CSKA Moscow,
Besiktas v Wolfsburg,
KUNDI C
AC Milan v Real Madrid,
Marseille v FC Zurich,
KUNDI D
Apoel Nicosia v FC Porto,
Atletico Madrid v Chelsea
Kimbembe kwa Real Madrid!!!!!
Klabu za England, Chelsea na Manchester United, leo zinaweza kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele Raundi ifuatayo ya Mtoano wakishinda mechi zao za leo.
Chelsea wanasafiri hadi Spain kucheza na Atletico Madrid wakiwa tayari wameshashinda mechi zao zote 3 za kwanza za Kundi D na mechi ya mwisho waliyocheza kwao waliibamiza Atletico Madrid bao 4-0.
Kipigo hicho kiliifanya Atletico Madrid, ambayo imeanza vibaya mno msimu huu hata kwenye Ligi ya kwao, kumtimua Kocha Abel Resino na wakamteua Quique Sanchez Flores kuchukua nafasi yake.
Mpaka sasa Atletico Madrid wana pointi moja tu katika Kundi D.
Katika Kundi hilo, FC Porto ndio wenye nafasi nzuri kuungana na Chelsea kuingia Raundi ifuatayo baada ya kuifunga APOEL Nicosia 2-1 mechi iliyokwisha na leo wanarudiana huko Visiwa vya Cyprus.
Katika Kundi B, Manchester United, ambao walikuwa Mabingwa wa Ulaya mwaka 2008 na kutolewa Fainali 2009, wako kileleni kwa kushinda mechi zao zote 3, ya mwisho ikiwa ushindi wa 1-0 huko Moscow walipoidonyoa CSKA Moscow wanaokutana nao leo Old Trafford.
Nafasi ya Pili kwenye Kundi hili B bado haijapata ufumbuzi na inagombewa na Wolfsburg, CSKA na hata Besiktas.
Leo, Besiktas inaikaribisha Wolsburg na Timu hizi zilitoka suluhu 0-0 mechi ya mwisho.
Gumzo na macho ya wengi leo ni mechi ya Kundi C ya marudiano kati ya AC Milan na Real Madrid baada ya AC Milan kuifunga Real mechi ya mwisho huko Spain Uwanja wa nyumbani wa Real wa Santiago Bernabeu 3-2 huku Pato akifunga bao la ushindi dakika 2 kabla mpira kumalizika.
Real leo itamkosa Mchezaji wa bei mbaya Ronaldo alieumia lakini Kaka yupo na leo itakuwa mechi yake ya kwanza kurudi kucheza Uwanjani San Siro tangu aihame AC Milan na kujiunga Real msimu huu.
Katika mechi nyingine ya Kundi hili C ni kati ya Marseille na FC Zurich huku Timu zote mbili zikiwa na matumaini ya kusonga mbele endapo kigogo mmoja kati ya Real na AC Milan akitetereka.
Marseille walliishinda FC Zurich 1-0 mechi ya kwanza.
Leo, katika Kundi A, Bordeaux wakimudu kuwafunga Bayern Munich watatinga Raundi ya Pili. Katika mechi yao ya kwanza ambayo Bordeaux walikosa penalti mbili na Bayern kulambwa Kadi 2 Nyekundu, Bordeaux walishinda 2-1.
Juventus wako nafasi ya pili Kundi hili na leo wapo Israel kucheza na Maccabi Haifa ambao wamefungwa mechi zote kwenye Kundi lao.

No comments:

Powered By Blogger