Tuesday 3 November 2009

Kroenke aendelea kununua hisa zaidi Arsenal
Mkurugenzi wa Arsenal, Stan Kroenke, ambae ni Mmarekani, ameendelea kununua na kulimbikiza hisa za Klabu ya Arsenal na sasa anamiliki hisa asilimia 29.6 na kisheria akizidisha zaidi ya hisa asilimia 29.99 basi atalazimika kutoa ofa ya kununua hisa za Klabu zote zilizobaki.
Siku za hivi karibuni, Mmarekani huyo ambae ni Bilionea na ni Mmiliki wa Klabu ya Mpira wa Vikapu huko Marekani, yaani NBA, Denver Nuggets, amenunua hisa 427 kwa bei ya Pauni 8,500 kila moja kwa jumla ya Pauni Milioni 3.6.
Stan Kroenke, aliebatizwa jina ‘Stan Mkimya’ [‘Silent Stan’] kwa vile amekataa kuelezea lolote kuhusu dhamira yake kuhusu kulimbikiza hisa za Arsenal, ndie kwa sasa Mmiliki wa hisa nyingi hapo Arsenal.
Wamiliki wengine wa hisa za Arsenal ni Tajiri wa Uzbekistan, Alisher Usmanov, mwenye asilimia 24, na wengine ni Danny Fiszman na Bibi Bracewell-Smith.
Beckham kutua AC Milan Januari 2010
Klabu ya David Beckham Los Angeles Galaxy ya Marekani na AC Milan zimethibitisha kufikia makubaliano kumruhusu Mchezaji huyo wa England kwenda kucheza kwa mkopo AC Milan mwezi Januari 2010 kwa miezi 6 wakati ambapo msimu wa Ligi ya MLS huko Marekani utakaposimama.
Lengo la Beckham kwenda kucheza huko Italia ni kukidhi matakwa ya Kocha wa England Fabio Capello ambae amemtaka Mchezaji huyo wa England, anaeshikilia rekodi ya kucheza mechi nyingi kwa Wachezaji wa mbele huko England, acheze Ligi yenye ushindani ili afikiriwe kuchukuliwa kuichezea England na hasa Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini zitakazoanza Juni 11, 2010.
Mwezi Januari, 2009, David Beckham alisaini mkataba wa miezi mitatu kuichezea AC Milan kwa mkopo na mkataba huo ukaongezwa hadi Ligi ya Serie A Italia ilipomalizika mwezi Mei, 2009 baada ya Beckham kuonyesha soka ya hali ya juu.
Kwa kuichezea AC Milan kwa kipindi hicho, Kocha Fabio Capello, ameendelea kumchukua Beckham kucheza Timu ya England.

No comments:

Powered By Blogger