Tuesday 23 March 2010

Arsenal wakata rufaa kupinga Kadi ya Vermaelen
Arsenal wamekata rufaa kwa FA kupinga Kadi Nyekundu aliyopewa Beki wao Thomas Vermaelen siku ya Jumamosi kwenye mechi ya Ligi Kuu waliyowafunga West Ham 2-0.
Refa Martin Atkinson alimtoa Vermaelen alipomchezea Guillermo Franco faulo alipokuwa akienda kufunga na hivyo kufungiwa mechi moja na anatakiwa aikose mechi ya Ligi ya Jumamosi inayokuja ambayo Arsenal wanasafiri kwenda kupambana na Birmingham.
Vermaelen na William Gallas ndio Masentahafu wa Arsenal msimu huu lakini Gallas amezikosa mechi kadhaa hivi karibuni baada ya kuumia na hivyo itabidi Wakongwe Sol Campbell na Mikel Silvestre wazibe mapengo ya Vermaelen na Gallas.
Rufaa hiyo ya Veermaelen inategemewa kusikilizwa leo.
Al Fayed aishambulia FIFA!!
Mmiliki wa Fulham, Mohamed Al Fayed, ameishambulia vikali FIFA kwa kukataa kutumia teknolojia ya kisasa katika Soka.
Kwa muda mrefu sasa Wadau wengi wa Soka wamekuwa wakiitaka FIFA itumie marudio ya mikanda ya video na elektroniki kwenye mistari ya magoli ili kuwasaidia Marefa kutoa uamuzi sahihi katika mechi lakini FIFA imegoma kufanya mapinduzi hayo kwa kudai utamu wa mpira unatokana na uamuzi na makosa ya Binadamu.
Al Fayed amefoka: “Nimepigia kelele hili kwa muda mrefu sasa! FIFA hawaelewi! Wao haiwaumizi, hawalipi chochote! Hawahisi chochote! Nani kawachagua? Sijui! Pengine kura za Afrika, nyingine Kathmandu [Nepal]! Kama ningekuwa na uwezo ningewafukuza wote!”
Al Fayed, Baba Mzazi wa Dodi aliefariki kwenye ajali ya gari pamoja na Princess Diana huko Paris mwaka 1997, ameapa kutayarisha mechi maalum kwenye Uwanja wa Klabu yake Fulham, Uwanja wa Craven Cottage, huku akitumia zana zote za kisasa kuwasaidia Marefa ili kuwadhihirishia FIFA na Rais wake Sepp Blatter kuwa kutumia teknolojia ya kisasa kunawezekana kabisa.
Nahodha Newcastle yuko Hospitali baada ya kupigwa mazoezini!
Nahodha wa Newcastle, Steven Taylor, amelazwa Hospitali ili kupata matibabu baada ya kuumizwa mazoezini kutokana na kupigana na Mchezaji mwenzake Andy Carroll.
Inadaiwa Taylor, ambae ndio kwanza amerudi mazoezini baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu, amevunjika taya na huenda akazikosa mechi zote za Newcastle za Ligi Daraja la Championship zilizobaki msimu huu.
Newcastle ndio vinara wa Ligi hiyo na wanategemewa kurudi tena Ligi Kuu baada ya kuporomoka msimu uliopita.
Habari za ugomvi huo hazijathibitishwa na Klabu ya Newcastle.

No comments:

Powered By Blogger