Friday 26 March 2010

Mourinho bubu!!
Kocha machachari na mwenye vituko vya hali ya juu wa Inter Milan, Jose Mourinho, ataendelea kutozungumza na Waandishi wa Habari kabla na baada ya mechi nyeti ya wikiendi hii ya Ligi Serie A watakapoumana na Timu ngumu AS Roma.
Uamuzi huo umethibitishwa na Klabu ya Inter Milan.
Mourinho aligoma kuongea na Waandishi mara baada ya kufungiwa mechi 3 kufuatia ishara ya mikono ya alama ya pingu aliyoitoa kwenye mechi na Sampdoria wakati Inter Milan ilipotoka sare 0-0 na Wachezaji wake wawili kupigwa Kadi Nyekundu kwenye mechi hiyo.
Tangu kifungo hicho cha mechi 3, mara pekee Mourinho alipoongea na Waandishi ni kwenye mechi ya UEFA CHAMPIONS LIGI.
Mourinho, ambae hana uhusiano mzuri na Vyombo vya Habari vya Italia, amekuwa akiwapeleka Wachezaji kuongea na Waandishi mara baada ya mechi.
Siku ya Jumatano, Inter Milan ilipoitandika Livorno bao 3-0, Mchezaji Ivan Cordoba ndie alieongea na Waandishi.
Platini bado ataka ulaji UEFA
Rais wa UEFA, Nyota wa zamani wa Ufaransa, Michel Platini, atasimama tena kugombea kwa mara ya pili nafasi ya Urais wa UEFA mwakani nafasi hiyo itakapopigiwa kura.
Platini, miaka 54, alichukua wadhifa huo wa Rais wa UEFA mwaka 2007 kutoka kwa Lennart Johansson na anategemewa kutopata Mpinzani kwenye uchaguzi wa mwakani.
Wakati huohuo, Platini amesema Brazil, England na Spain ndizoTimu zinazotegemewa kushinda Kombe la Dunia ambazo Fainali zake zitachezwa Juni 11 hadi Julai 11 huko Afrika Kusini.
Brazil wameshawahi kuwa Mabingwa wa Dunia mara 5, England mara moja na Spain, ambao ndio Mabingwa wa Ulaya, hawajawahi kuwa Mabingwa wa Dunia.
Hata hivyo, Platini amezitaja Nchi nyingine, anazotegemea kuwa ngumu na tishio kwa Vigogo hao watatu aliowataja, ni Nchi za Argentina, Ufaransa, Uholanzi, Italy, Ivory Coat na Ureno.
Celtic ya Scotland yamtimua Meneja wake!!
Klabu Kongwe ya huko Scotland, Celtic, imemfukuza kazi Meneja wake Tony Mowbray kufuatia kipigo cha Timu hiyo cha 4-0 mikononi mwa St Mirren siku ya Jumatano.
Kipigo hicho cha 4-0 kimewafanya Celtic wawe pointi 10 nyuma ya Mahasimu wao wakubwa Rangers walio vinara wa Ligi Kuu Scotland.
Nahodha wa zamani wa Celtic Neill Lennon ambae amekuwa akifanya kazi Klabuni hapo kama Kocha amepewa wadhifa wa Meneja wa muda hadi hapo Klabu itakapompata mtu wa kudumu.

No comments:

Powered By Blogger