Friday 26 March 2010

Bifu la Mancini v Moyes: Sasa Mancini ana kesi na FA!!
Roberto Mancini ameshitakiwa na FA kwa kosa la kutokuwa na mwenendo mzuri kufuatia kufarakana kwake na Meneja wa Everton David Moyes katika mechi ya Ligi Kuu hapo juzi kati ya Manchester City na Everton Uwanja wa City of Manchester ambayo Everton walishinda 2-0.
Bosi huyo wa Manchester City alimvaa Moyes aliekuwa ameushika mpira uliotoka nje ili kutoa nafasi Timu yake ibadili Mchezaji lakini Mancini akataka kumpora mpira huo na ikatokea mshikemshike ulioamuliwa na Mwamuzi wa Akiba howard Webb na Walinzi wa Uwanjani hapo.
Baada ya Mancini na Moyes kutenganishwa Refa wa mechi hiyo Peter Walton aliwatoa nje ya Uwanja wote Mancini na Moyes.
Ingawa David Moyes amepona mashitaka, FA imemwandikia barua kumkumbusha majukumu na mwenendo wake kama kiongozi.
Moyes amesema tukio hilo ni dogo na Mancini alimwomba radhi mara baada ya kutokea na yeye hana kinyongo chochote.
Mancini amepewa mpaka Aprili 6 kujibu mashitaka hayo na Kamisheni ya Sheria itakaa Aprili 19 kutoa uamuzi.
Nani asaini Mkataba wa Miaka 4 Man United
Winga wa Manchester United kutoka Ureno, Nani, miaka 23, amesaini Mkataba mpya wa miaka minne na Klabu yake.
Nani, ambae alijiunga Man United mwaka 2007 akitokea Sporting Lisbon, alikuwa amebakisha miaka miwili katika Mkataba wake wa sasa.
Meneja wa Man United, Sir Alex Ferguson, akithibitisha habari hizo, alisema: “Ameibuka kama kipaji na amepata maendeleo makubwa hapa!”
Mwenyewe Nani, ambae ameshachezea mechi 97 na kuifungia Man United mabao 12, ametamka: “Nimefurahia Mkataba mpya! Ni ndoto iliyotimia kuichezea Man United! Makocha wamenifundisha mengi na nacheza miongoni mwa Wachezaji bora duniani! Natazamia kubeba Vikombe vingi na Timu hii!”

No comments:

Powered By Blogger