Thursday, 25 March 2010

Pompey 0 Chelsea 5
Jana, kwenye Ligi Kuu, Chelsea iliiwasha Timu taabani Portsmouth mabao 5-0 na kuipiku Arsenal kwenye nafasi ya pili.
Manchester United wanaongoza wakiwa na pointi 69, Chelsea wa pili pointi 68 na Arsenal ni wa tatu wakiwa na pointi 67. Kila Timu imecheza mechi 31 na kubakiza mechi 7.
Mabao ya Chelsea yalifungwa na Drogba, bao mbili, Malouda, bao mbili, na Lampard moja.
Katika mechi nyingine za jana za Ligi Kuu matokeo ni:
Man City 0 Everton 2
Blackburn 2 v Birmingham 1
Aston Villa 1 v Sunderland 1
Beckenbauer: Rooney ni hatari!!!
Rais wa Bayern Munich ambae alikuwa Supastaa wa Ujerumani zamani, Franz Beckenbauer, amekiri Wayne Rooney ndie hatari kubwa kwao katika kiu yao ya kutwaa Ubingwa wa Ulaya.
Beckenbauer amesema Rooney anaifanyia kazi nzuri Timu yake Manchester United na kufunga goli 33 katika msimu si kitu kidogo kwa Soka la siku hizi.
Veterani huyo amesema: “Ni Mchezaji hatari! Sisi Bayern tunamwogopa na tunamgwaya kucheza nae kwenye Robo Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI!”
Msimu huu,Manchester United na Bayern Munich zitakutana Robo Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI na mechi hizo ni kumbukumbu kwa wengi Fainali ya mwaka 1999 ya UEFA CHAMPIONS LIGI Man United walipoibwaga Bayern Munich 2-1 kwa goli mbili za dakika za majeruhi zilizofungwa na Teddy Sheringham na Ole Gunnar Solskjaer.
Man United na Bayern Munich zitacheza mechi ya kwanza ya UEFA CHAMPIONS LIGI huko Ujerumani Machi 30 na marudiano ni Old Trafford Aprili 7.
Vilevile, Beckenbauer amesema Rooney anao uwezo wa kuiletea ushindi England huko Afrika Kusini katika Fainali za Kombe la Dunia.
Nae Meneja wa zamani wa Bayern Munich Jurgen Klinsmann amesema: “Rooney ni mkali msimu huu. Ametulia, anajiamini na akiendelea hivi basi atachaguliwa Mchezaji Bora Ulaya!”
Pompey waruhusiwa kuuza Wachezaji
Portsmouth wamepewa kibali maalum na Ligi Kuu kuuza Wachezaji wao nje ya dirisha la uhamisho ili kupoza ukata unaoikabili Klabu hiyo.
Klabu hiyo ambayo tayari imeshakatwa pointi 9 na ipo mkiani kwenye wa msimamo wa Ligi na hilo, bila shaka, litawashusha Daraja,wameruhusiwa kuuza Wachezaji lakini hawaruhusiwi kuchezea Timu za kwanza za Klabu za Ligi Kuu.
Hata hivyo Msimamizi maalum wa Klabu hiyo Andrew Andronikou amesema: "Ingawa kuuza Wachezaji ni moja ya mikakati lakini kwa sasa hatulazimiki kufanya hivyo kwani kufika kwetu Nusu Fainali Kombe la FA kumetupa pesa za kujiendesha.”
Pompey waliomba kuuza Wachezaji mwezi Februari lakini waligomewa na Ligi Kuu.
Klabu hiyo imepewa masharti ya kuuza Wachezaji nayo ni:
-Wachezaji hawaruhusiwi kuchezea Timu za kwanza za Ligi Kuu hadi msimu umalizike.
-Wanaweza kuingia mkataba na Klabu nyingine kwa sasa ili Mchezaji ahamie huko mwishoni mwa msimu.
-Mauzo ya Mchezaji yeyote lazima yaidhinishwe na FIFA.
Kawaida kuna madirisha mawili ya uhamisho, moja ni Januari 1 hadi 31 na la pili ni Juni 1 hadi Agosti 31.
Mwezi Januari Portsmouth waliuza Wachezaji watatu.

No comments:

Powered By Blogger