Tuesday, 30 September 2008


Aab Aalborg v Manchester United: Timu zinazoongozwa na Mameneja toka Scotland

Leo katika mechi ya KUNDI E ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE Mabingwa watetezi Manchester United wako nchini Denmark kwenye mji mdogo uitwao Aalborg kupambana na timu ndogo lakini ndio Mabingwa wa Denmark Aab Aalborg.

Mechi hii itakayoanza saa 3 dakika 45 usiku, saa za bongo, itachezwa kwenye Uwanja uitwao Energi Nord Arena wenye uwezo wa kuchukua Watazamaji 10,000 tu.

Aab Aalborg ilitoka sare kwenye mechi ya kwanza ya Kundi hili ilipocheza ugenini na Celtic huko Scotland. Kipa wa Aab Alborg Karim Zaza toka Morocco alikuwa shujaa alipookoa penalti kwenye mechi hiyo.

Aab Aalborg inaongozwa na Meneja ambae kama Meneja wa Man U Sir Alex Ferguson ni mtu wa Scotland. Bruce Rioch, mwenye umri wa miaka 61, ni Mchezaji wa zamani wa Aston Villa na ameshawahi kuwa Meneja wa timu za LIGI KUU Middlesbrough na Arsenal.

Bruce Rioch ndie aliemsaini Dennis Berkamp na mwaka 1996 akiwa Meneja wa Arsenal waliwahi kuwafunga Man U kwa bao la Bergkamp.

Kikosi cha Aab Aalborg kina vijana wengi wa Timu ya Taifa ya Denmark ya umri wa chini ya miaka 21 ingawa kuna Wachezaji kadhaa toka nje ya nchi kama Kipa Karim Zaza [Morocco], Marek Saganowski (Poland), Andreas Johansson (Sweden) na Michael Beauchamp (Australia).

Wengi wanahisi hii ni mechi kati ya Klabu ndogo na maskini zidi ya Klabu kubwa na tajiri. Hebu linganisha: Uwanja wa Aalborg, Energi Nord Arena, una uwezo wa kuchukua Watazamaji 10,000 tu wakati Old Trafford wa Man U unapakia watu zaidi ya 76,000! Dau lililolipwa kumnunua Dimitar Berbatov toka Tottenham kuja Man U la Pauni Milioni 30 ni bajeti ya kuiendesha Aab Alborg kwa miaka 7!

Juu ya yote hayo, Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson amesema: 'Timu za Denmark ni wapiganaji! Hatuwadharau hivyo ntashusha kikosi changu kamili.'

No comments:

Powered By Blogger