Wednesday 1 October 2008

BAADA YA USHINDI WA JANA:

Wenger asherehekea ushindi!!!

Meneja wa Arsenal Arsena Wenger, baada ya mstuko wa kupigwa na 'vibonde' Hull City Jumamosi uliomfanya aweweseke hadi kukosea kutaja timu iliyomfunga na kuiita West Brom na kuahidi shoka litatembea kwa Wachezaji kwenye mechi ya jana, alikuwa mtu mwenye furaha kubwa jana baada ya ushindi wa mabao 4-0.

Wenger hakutimiza ahadi yake ya shoka ingawa hakumchezesha Eboue na badala yake Samir Nasri alianza na dakika ya 64 Eboue akambadilisha Nasri.

Wenger alinena kwa furaha: 'Sikufanya mabadiliko kwani sikutaka nionekane natoa adhabu kwa Wachezaji. Ni bora uipe timu nafasi ijirekebishe makosa!'

Sir Alex Ferguson akumbwa na majeruhi!!!

Ingawa Mabingwa wa Ulaya, Manchester United, wamefurahia ushindi wa mabao 3-0 ugenini huko Aalborg, Denmark walipoitwanga Aab Aalborg, ushindi huo pengine umekuja kwa gharama kubwa kutokana na kuumia kwa Wachezaji muhimu sana kwa timu.

Paul Scholes aliumia goti dakika ya 16 tu ya mchezo na akatolewa kwa machela na nafasi kuchukuliwa na Ryan Giggs. Mwishoni mwa mechi Scholes alionekana akitembelea kwa magongo. Ferguson alisema huenda Scholes akawa nje ya uwanja kwa wiki hadi 8.

Pigo la pili lilikuwa kuumia enka kwa Wayne Rooney ingawa taarifa zilisema kutolewa kwake uwanjani ilikuwa ni tahadhari tu na maumivu yake si ya kutisha kama ya Scholes. Nafasi ya Rooney kwenye mechi hiyo ilichukuliwa na Carlos Tevez.

Pigo la tatu ni kuumia kwa Beki chipukizi Rafael kutoka Brazil ambae alikuwa akianza mechi kubwa kwa mara ya kwanza na nafasi yake kushikwa na Wes Brown.

Nae Dimitar Berbatov aliefungua akaunti yake ya kufunga magoli kwa Man U hapo jana alipofunga bao 2 amemkosha Ferguson aliemsifia sana: 'Berbatov amefunga magoli mawili maridadi sana! Magoli hayo ya mwanzo kuifungia Man U yatampa morali kubwa!'

No comments:

Powered By Blogger