Monday 20 October 2008

FERGUSON AMWOKOA MTANGAZAJI!

Mtangazaji wa Michezo wa Kituo cha TV maarufu huko Uingereza ITV, Jim Rosenthal, ambae aliondolewa kazini bila kutarajia ameokolewa na Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson na sasa amerudishwa tena kibaruani.
Jim Rosenthal, mwenye umri wa miaka 60, ambae ameitumikia ITV kwa miaka 28, aliambiwa mwezi Januari mwaka huu kuwa mkataba wake ukiisha haongezewi tena!
Alionekana kwenye luninga kwa mara ya mwisho mwezi Juni mwaka huu.
Hivi karibuni, Sir Alex Ferguson, akiwa mgeni mwalikwa kwenye hafla ya hisani, alitoa ombi maalum kwa wageni wenzake waalikwa ambao wengi walikuwa ni nyota mbalimbali kwenye michezo na watu maarufu: 'Jim Rosenthal alikuwa Mtangazaji bora wa TV. Sasa hana kazi. Naomba kila mtu awaandikie ITV na kuwataka arudishwe kazini. Ni Mtangazaji bora sana lakini Mabosi wake wanasema ni mzee!'
Sasa Jim Rosenthal amepewa mkataba mpya wa miaka minne na atasimamia mechi za Kombe la FA na Masumbwi.
Mwenyewe Jim Rosenthal anasema: 'Ni kweli Sir Alex Ferguson amenisaidia sana! Nilipata mstuko mkubwa nilipoambiwa sina kazi tena! Utangazaji ni maisha yangu! Ferguson anasaidia watu wengi sana lakini hataki ajulikane kwa hilo! Alipotamka maneno yale mazuri kuhusu mimi kwenye ile hafla ilinigusa sana na vitu kama hivi mabosi wanasikiliza! Nilikuwa na wakati mgumu lakini huo ndio wakati unaogundua nani rafiki wako wa kweli!'
Na, bila shaka, Sir Alex Ferguson ni rafiki yake bora na wa kweli kikweli!

No comments:

Powered By Blogger