Sunday, 19 October 2008

'NYODO' DROGBA:
=Ateuliwa tena kuwa miongoni mwa wagombea MCHEZAJI BORA AFRIKA 2008 licha ya kususia mwaka 2007!

=Adai angempiga ngumi Nemanja Vidic wa Man U!

Didier Drogba wa Chelsea na Nchi ya Ivory Coast ameteuliwa kuwa miongoni mwa wagombea wa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika 2008 licha ya kususia sherehe za kukabidhi Tuzo hiyo mwaka jana huko nchini Togo ambako alitegemewa kushinda Tuzo hiyo kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuitwaa ile ya mwaka 2006.
Kususia kwake kulifanya Tuzo hiyo akabidhiwe Frederic Kanoute wa Mali.
Drogba alisusia kwa sababu sherehe hizo zilikuwa zinafanyika siku mbili tu kabla Nchi yake Ivory Coast ikutane na Guinea kwenye Robo Fainali ya Kombe la Afrika wakati huo fainali hizo za Kombe la Afrika zilikuwa zinachezwa Misri.
Badala yake alimtuma mkewe kumuwakilisha.
Licha ya kususa, alidai vilevile hataki kuhusishwa tena na Tuzo hiyo.
Vilevile, Drogba ameibua upya tena uhasama baada ya kuandika kwenye kitabu cha maisha yake kilichotolewa majuzi kwamba ingekuwa bora angempiga ngumi Beki wa Manchester United Nemanja Vidic kwenye Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE wakati Chelsea waliposhindwa na Manchester United na kuukosa Ubingwa wa Klabu za Ulaya.
Drogba alilambwa kadi nyekundu kwenye mechi hiyo baada ya kuinua mkono na kumpiga kibao Vidic na hivyo kukosa kupiga penalti ambazo ziliizamisha timu yake Chelsea.
Didier Drogba pamoja na mwenzake wa Chelsea Michael Essien wa Ghana, Emmanuel Adebayor wa Togo na Arsenal, Wamisri Amr Zaki kutoka Klabu ya Zamalek ya Misri [kwa sasa yuko kwa mkopo Wigan] na Mohamed Aboutrika wa El Ahly ya Misri ndio watakaogombea TUZO YA MCHEZAJI BORA AFRIKA 2008.

No comments:

Powered By Blogger