Sunday 19 October 2008

LIGI KUU: VIGOGO WAANZA KUJIKITA JUU!!!

Wanaongoza Chelsea wakifuatiwa na Liverpool, Arsenal na Man U!

Baada ya Chelsea, Liverpool na Arsenal kucheza mechi 8 kila mmoja huku Mabingwa Man U wakiwa wamecheza mechi moja pungufu, Chelsea ndie aliejikita katika uongozi wa LIGI KUU akiwa na pointi 20 sawa na Liverpool lakini Chelsea anaongoza kwa idadi kubwa ya magoli.
Wote, Chelsea na Liverpool, hawajapoteza hata mechi moja ingawa wote wametoka suluhu mechi mbili.
Timu hizi zitakutana uso kwa uso wiki ijayo wakati zitakapopambana Jumapili tarehe 26 Oktoba 2008, Stamford Bridge ambayo ni ngome ya Chelsea.
Anaefuata katika msimamo wa ligi ni Arsenal mwenye pointi 16 na tayari ameshafungwa mechi 2 na kutoka suluhu moja.
Mabingwa wa LIGI KUU, Manchester United, wako nafasi ya nne na wamecheza mechi moja pungufu na wana pointi 14.
Mechi ambayo bado wanayo mkononi na ambayo hawajaicheza ni ile dhidi ya Fulham iliyotakiwa ichezwe nyumbani kwa Man U, Old Trafford, lakini iliahirishwa kwa sababu Man U alikuwa kwenye mechi ya UEFA SUPER CUP waliyocheza na Zenit St Petersburg.
Mechi hii kiporo bado haijapangwa tarehe.
Endapo Man U watacheza hiki kiporo na kushinda basi watashika nafasi ya 3 na kuwa nyuma ya Chelsea na Liverpool kwa pointi 3 tu.
Leo, Timu mpya msimu huu iliyopanda daraja na inayostaajabisha wengi, Hull City, hasa baada ya kuzipiga Arsenal na Tottenham zote zikiwa nyumbani kwao, inashuka dimbani kupambana na West Ham inayosuasua.
Hull City wakishinda mechi ya leo dhidi ya West Ham, mechi inayochezwa kwake Uwanja wa KC, basi atakuwa na pointi 17 na atachupa hadi nafasi ya 3 na kuzipiku Arsenal na Man U ingawa kwa Man U atakuwa amemzidi mchezo mmoja.
Mechi nyingine inayochezwa leo ni ile ya Timu zinazoshika mkia, Stoke City iliyo nafasi ya 19 wakiwa na pointi 4 na Tottenham walio nafasi ya 20 na ya mwisho wakiwa na pointi 2 tu.
Mechi hii inachezewa Uwanja wa Britannia nyumbani kwa Stoke City.

No comments:

Powered By Blogger