Saturday 29 August 2009

Man U 2 Arsenal 1
Diaby aipa ushindi Man U!!!
Old Trafford leo iliwaka moto, ingawa Timu zote zilionekana kuwa kidogo chini ya kiwango, baada ya Manchester United na Arsenal kupambana kwenye mechi ya Ligi Kuu na Man U kutoka na ushindi wa 2-1.
Arsenal, walioonekana kuwa juu kidogo kipindi cha kwanza, walipata bao kupitia Arshavin dakika ya 41 alipopiga shuti kali ambalo Kipa Foster alishindwa kuzuia.
Mpaka mapumziko Man U 0 Arsenal 1.
Kipindi cha pili, Man U waliweza kucheza vizuri zaidi na dakika ya 58 Wayne Rooney akaangushwa na Kipa Almunia na Refa Mike Dean akaamua ni penalti.
Rooney alipiga penalti hiyo na kufunga.
Dakika 5 baadae Man U walipata frikiki upande wa kulia na Giggs akaidondosha katikati ya goli na ndipo Diaby, akiwa hayuko kwenye presha yeyote, akapiga kichwa na kujifunga mwenyewe.
Dakika 90 zilipomalizika zikaongezwa dakika 5 za nyongeza na Arsenal walimudu kufunga bao muda huo kupitia van Persie lakini Mshika Kibendera alikuwa tayari ameashiria ofsaidi kwa Gallas ambae alitoa pasi kwa van Persie.
Uamuzi huo, ulioonekana ni sahihi kwenye marudio ya video, ulimkasirisha Arsene Wenger na akaipiga teke chupa ya maji na ndipo Mwamuzi wa Akiba alipomwita Refa Mike Dean alieamuru Wenger atoke nje Uwanjani.
Kichekesho kilikuwa Wenger [pichani] akaenda moja kwa moja kusimama mbele ya Washabiki wa Man U waliokuwa wakimshangilia.
Vikosi:
Manchester United: Foster, O’Shea, Brown, Vidic, Evra, Fletcher, Carrick, Giggs, Nani, Rooney, Valencia.
Akiba: Kuszczak, Berbatov, Anderson, Owen, Neville, Park, Scholes
Arsenal: Almunia, Sagna, Gallas, Vermaelen, Clichy, Eboue, Denilson, Song Billong, Diaby, Arshavin, van Persie.
Akiba: Mannone, Eduardo, Ramsey, Silvestre, Wilshere, Gibbs, Bendtner.
Refa: Mike Dean (Wirral)

No comments:

Powered By Blogger