Friday 28 August 2009

Villa nje, Fulham, Everton wapeta EUROPA LIGI!!!
Licha ya kufungwa ugenini bao 1-0 na Amkar Perm ya Urusi, Fulham imefanikiwa kuingia hatua ya Makundi ya EUROPA LIGI kwa jumla ya mabao 3-2 huku wenzao Everton wakijumuika nao baada ya pia kuwa ugenini na kutoka suluhu ya 1-1 na Sigma Olomouc ya Czech Republic na kutinga kwenye Makundi kwa jumla ya mabao 5-1.
Kwa Aston Villa, licha ya kushinda uwanjani kwao 2-1 dhidi ya Rapid Vienna ya Austria, Villa imebwagwa nje ya EUROPA LIGI kwa bao la ugenini kwani ilifungwa mechi ya kwanza bao 1-0 na hivyo jumla ya mabao kuwa 2-2 katika mechi mbili.
Droo ya kuamua Timu zipi zitakuwa Kundi lipi itafanywa leo huko Monaco kabla ya mechi ya leo kugombea SUPER CUP kati ya Bingwa wa UEFA CHAMPIONS LEAGUE, Barcelona, na Bingwa wa UEFA CUP, Shakhtar Donetsk.
Klabu za Uingereza zakwepa Vigogo Ulaya UEFA CHAMPIONS LEAGUE
Klabu 5 za Uingereza zimewekwa kwenye Makundi ambayo Wadau wengi wamedai ni “laini kidogo” baada ya kuepuka kupangwa na Timu Vigogo wa Ulaya. Manchester United ambao walifika Fainali msimu uliopita wapo pamoja na CSKA Moscow, Besiktas na Wolfsburg KUNDI B.
Liverpool watamenyana na Lyon, Fiorentina na Debrecen wakati Chelsea wapo na Porto, Atletico Madrid na APOEL Nicosia.
Arsenal wamepangiwa na AZ Alkmaar, Olympiakos na Standard Liege wakati Rangers ya Scotland itacheza na Stuttgart, Sevilla na Unirea Urziceni.
Klabu za England zimekwepa kuwekwa na Real Madrid na Inter Milan huku Real akiwa Kundi moja na AC Milan, Marseille na FC Zurich.
Inter Milan yuko pamoja na Barcelona, Dynamo Kiev na Rubin Kazan.
Msimu uliokwisha Chelsea walitolewa nje na Brcelona kwenye Nusu Fainali kwa bao la Andres Iniesta la dakika za majeruhi na Mkurugenzi Mtendaji wao Peter Kenyon alizungumza baada ya upangaji Makundi na kusema: “Tunaanza upya na siku zote tunataka twende mbele zaidi. Hamna mechi rahisi au Kundi laini lakini tumewakwepa Vigogo!!”
Manchester United, kwa kuwa Kundi moja na CSKA Moscow, watarudi tena Uwanja wa Luzhniki walipowatoa Chelsea Fainali ya 2008 na kuwa Bingwa wa Ulaya na Mkuurugenzi Mkuu wa Klabu hiyo David Gill ametamka: “Kwa ujumla, tunafurahia Kundi letu. Tuna shauku kubwa kurudi tena Moscow baada ya furaha ya 2008!”
Lakini, Sir Alex Ferguson, Meneja wa Man U, alisema: “CSKA sasa wamejijenga sana na mechi za kuchezea Uturuki ni ngumu siku zote. Pia tunajua ubora wa Wolfsburg na mafanikio yao Bundesliga msimu uliopita.”
Nae, Mkurugenzi Mkuu wa Liverpool, Christian Purslow, amesema: “Tumefurahia!”
Mkuu wa Arsenal, Ivan Gazidis, alionyesha tahadhari kuhusu KUNDI H ambalo wao wapo na kutamka: “Wengine wataangalia na kusema Arsenal atapita lakini tupo makini. Itakuwa ngumu ila tutatimiza kazi yetu.”
Yapo Makundi Manane yenye Timu 4 kila moja na mechi zitachezwa mtindo wa Ligi wa nyumbani na ugenini huku mechi za kwanza zikichezwa Septemba 15 na 16.
Washindi wanane wa kila Kundi pamoja na Washindi wa pili wataingia hatua ya mtoano huku washindi wa tatu wakiingizwa EUROPA LIGI.
Fainali itachezwa Uwanja wa Real Madrid Bernabeu Stadium tarehe 22 May 2010 ambayo ni Jumamosi tofauti na hapo nyuma Fainali kuchezwa Jumatano.
UHAMISHO LIGI KUU ENGLAND!!!!!
Zikiwa zimebaki siku chache kabla dirisha la uhamisho halijafungwa hapo Agosti 31, spidi ya uhamisho imepamba moto huku Klabu nyingi bado zikichacharika kusaka Wachezaji.
Baadhi ya biashara zilizokamilika hivi karibuni ni pamoja na uhamisho wa Mlinzi na Nahodha wa Manchester City Richard Dunne, miaka 29, kuhamia Aston Villa.
Aston Villa pia imemchukua Stephen Warnock, miaka 27,kutoka Blackburn Rovers kwa mkataba wa miaka minne.
Warnock, anaeweza kucheza kama Kiungo au Beki wa kushoto, alijiunga na Blackburn mwaka 2007 akitokea Liverpool.
Mlinzi wa Portsmouth Sylvain Distin, miaka 31, amejiunga na Everton kwa mkataba wa miaka mitatu na ada ambayo haikutajwa.
Nao Wachezaji wa Middlesbrough iliyoshushwa Daraja msimu uliokwisha, Robert Huth, mlinzi kutoka Ujerumani na Tuncay Sanli wa Uturuki, wamejiunga na Stoke City.
Blackburn Rovers wamemsaini Pascal Chimbonda kwa mkataba wa miaka miwili kutoka Tottenham Hotspur.
Bayern Munich wamchota Robben!
Real Madrid wamekubali kumuuza Winga wa zamani wa Chelsea, Mdachi Arjen Robben, kwa Bayern Munich kwa ada ya Pauni Milioni 22.
Robben, miaka 25, alitegemewa kuhama Real tangu Klabu hiyo iwanunue Cristiano Ronaldo na Kaka.
Nae Bosi mkubwa wa Bayern Munich, Hoeness, ametamka: “Robben ataimarisha Timu. Yeye akicheza Winga kulia na Ribery kushoto Timu itakuwa bomba!”

No comments:

Powered By Blogger