Saturday, 29 August 2009

MECHI YA LEO: Ferguson v Wenger, Wanasemaje?
Leo ni Bigi Mechi kati ya Manchester United na Arsenal Timu zinazotambulika huko England kuwa ni miongoni mwa Timu Vigogo Wanne wa Ligi Kuu wengine wakiwa ni Liverpool na Chelsea.
Ni kawaida kabla ya mechi zinazowakutanisha Vigogo hao, Waandishi kuwabana Mameneja wa Timu hizo na kutaka maoni na mitazamo yao.
Mechi kati ya Manchester United na Arsenal inawakutanisha Mameneja Sir Alex Ferguson wa Manchester United na Arsene Wenger wa Arsenal ambao ndio Mameneja waliodumu muda mrefu wakiwa uongozini kwenye Ligi Kuu England kupita wengine wote.
Mbali ya hilo, ushindani wa Klabu hizi, siku za nyuma, ulikuwa mkubwa sana kiasi cha kujenga uhasama ndani na nje ya Uwanja.
Lakini, Sir Alex Ferguson, licha ya kukiri kuwa msimu huu Arsenal watakuwa moja ya Timu zinazostahili kutwaa Ubingwa, amesema haamini ushindani huo utaibua tena uhasama uliokuwepo siku za nyuma.
Wengi wanaamini kushindwa kwa Arsenal kwa misimu kadhaa ya hivi karibuni kutwaa Ubingwa, kitu ambacho Wenger anakiunga mkono, ndiko kumesababisha uhasama upungue lakini Ferguson anapinga hilo. Ferguson anasema: “Sikubaliani na hilo! Nadhani kitu kikubwa ni kwamba Wachezaji wamebadilika! Sasa hatuna Roy Keane na wao hawana Patrick Viera! Hao wawili walikuwa ni cheche na Manahodha waliotawala Timu zao! Uhasama kati yao ulisukumwa hadi kwa Mameneja!”
“Vilevile……” Ferguson anaongeza. “……mimi na Wenger tuko hapa muda mrefu na ni kitu cha kawaida watu kutofautiana. Kwa sasa Mameneja wanakuja, siku mbili baadae hawapo! Nadhani sisi wawili tutaondoka pamoja jua likichuwama!”
Kuhusu Arsenal ya msimu huu, Ferguson anasema ni Timu nzuri na itakuwemo kwenye kinyang’anyiro cha Ubingwa.
Nae Wenger amekiri kuwa Ulimwengu wote wa soka unaichukulia mechi ya leo kama kipimo kwa Arsenal hasa baada ya kuanza msimu kwa kishindo kwa kushinda mechi zao zote mbili za Ligi Kuu walipoiua Everton 6-1 nyumbani kwa Everton Goodison Park na kuifumua Portsmouth 4-1 Emirates Stadium na pia kuitoa Timu ngumu Celtic kwenye UEFA CHAMPIONS LEAGUE kwa kuifunga mechi zote mbili kwa mabao 2-0 na 3-1.
Lakini katika mechi ya leo Arsenal itaukosa mhimili wao Nahodha Cesc Fabregas ambae ni majeruhi na Wenger ameelezea hilo.
Anasema: “Cesc anatupa utulivu. Yeye ni bingwa wa kuusoma mchezo na pia Mfungaji. Lakini nguvu za pamoja za Diaby, Denilson na Song itafidia pengo lake.”
Wenger ameongeza kwa kuisifia ngome yake ambayo kwa sasa inaongozwa na Masentahafu Gallas na Vermaelen.
Vilevile Wenger alisema kwa sasa Manchester United iko kipindi cha mpito baada ya Ronaldo kuondoka na kufananisha na kuondoka Arsenal kwa Thierry Henry kwenda Barcelona mwaka 2007.
Wenger anasema: “Mchezaji akiwa na nguvu kwenye Timu, mara nyingi mchezo huchezwa kupitia kwake. Kwetu, hakuna mtu aliebisha au kusita kumpasia Henry. Mchezaji wa aina hiyo akiondoka, wengine wanaibuka lakini inachukua muda. Kwetu walitokea Adebayor na Hleb. Naamini Man U wana dosari kumkosa Ronaldo lakini wataibuka wengine. Na wapo Rooney na Berbatov wenye uwezo kufunga goli 20 kila mmoja.”
Wenger pia akamsifia Michael Owen na kumwelezea kuwa ni mjanja, Mfungaji mzuri sana na mwenye akili kwenye boksi.

No comments:

Powered By Blogger