Tuesday, 30 March 2010

Drogba kifungo mechi 2 UEFA!
Mshambuliaji wa Chelsea, Didier Drogba, ameadhibiwa kufungiwa mechi 2 za Mashindano ya UEFA baada ya kupewa Kadi Nyekundu katika mechi ya UEFA CHAMPIONS LIGI kati ya Chelsea na Inter Milan Uwanjani Stamford Bridge ambayo Chelsea alifungwa 1-0.
Drogba alipewa Kadi hiyo dakika ya 87 kwa kumtimba Mchezaji wa Inter Milan Thiago Motta.
Msimu uliokwisha katika mechi ya Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI uwanjani Stamford Bridge kati ya Chelsea na Barcelona ambayo Barcelona walisawazisha bao dakika za majeruhi na kufanya mechi iwe 1-1 na hivyo kutinga Fainali kwa goli la ugenini, Drogba alimvaa Refa Tom Henning Ovrebo na kumtolea maneno makali mara tu baada ya filimbi ya mwisho.
Kwa kitendo hicho, Drogba alifungiwa mechi 4 lakini zikapunguzwa hadi 3 na mechi mbili zikawekwa kiporo kuchunguza mwenendo wake.
Safari hii, kwa kosa hilo la kutolewa kwenye mechi na Inter Milan, UEFA ingeweza kumfungia mechi 2 na kuziongeza hizo mechi mbili alizowekewa kiporo lakini UEFA imeamua kumfungia mechi mbili 2 na kuongeza muda wake wa kuwa chini ya uangalizi uwe hadi miezi 24 na hivyo utaisha Julai 2013.
Drogba amepewa siku 3 kukata rufaa adhabu hizo.
Martinez alaumu Refa kwa kufungwa!
Man City 3 Wigan 0
Bosi wa Wigan Roberto Martinez amemlaumu Refa Stuart Attwell, miaka 27, kwa kumpa Kadi Nyekundu Mchezaji wake Gary Caldwell huku mechi ya Ligi Kuu kati ya Manchester City na Wigan ikiwa 0-0 na hivyo kutoa mwanya kwa Man City kushinda 3-0, bao zote zikiingizwa na Carlos Tevez katika kipindi cha pili katika muda uliochukua dakika 12 tu kwa bao zote kutinga.
Martinez amedai Refa Stuart Atwell, ambae ndie Refa mwenye umri mdogo kupita Refa yeyote kwenye Ligi Kuu, hakuiona rafu aliyotenda Caldwell kwa Tevez na hivyo hakustahili kutoa Kadi.
Martinez alifoka: “Kutoa Kadi Nyekundu ni lazima uwe na uhakika. Ukiangalia marudio ya tukio la rafu utaona ile si rafu! Refa hakuona, hivyo kutoa uamuzi kwa kitu usichoona ni udanganyifu!”
Kauli hizo za Martinez sasa zimefika kwenye ofisi za FA na wamesema wanachunguza na watatoa uamuzi wao wa kumchukulia hatua muda si mrefu ujao.
Bayern yaahidi kumdhibiti Rooney
Kocha wa Bayern Munich Loius van Gaal amesema ana uhakika Timu yake ina uwezo wa kumdhibiti Wayne Rooney leo watakapocheza na Manchester United Uwanja wa Allianz Arena, nyumbani kwa Bayern, kwenye mechi ya kwanza ya Robo Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI.
Van Gaal amedai ingawa Rooney ni Mchezaji bora sana wao wana uwezo wa kumkontroli na kushinda mechi hiyo.
Van Gaal amesema: “Tuna uwezo wa kuishangaza Timu yeyote! Bayern si Timu kubwa kama Man United lakini uwezo upo wa kufikia gemu yao!”
Nae Sir Alex Ferguson amesema wao wameongezeka ubora wa kucheza mechi za Ulaya na sasa wana ujuzi, uvumilivu na utulivu wa kushinda ugenini.
Mpaka sasa Man United, kwenye Mashindano ya UEFA CHAMPIONS LIGI, wameshinda mechi zao 7 za mwisho, hawajafungwa katika mechi 17 za ugenini na wameshinda mechi zao zote 4 walizocheza ugenini Msimu huu.
Newcastle wapiga hodi Ligi Kuu
Newcastle ambayo iliporomoshwa Daraja kutoka Ligi Kuu msimu uliokwisha huenda wikiendi hii inayokuja wakajihakikishia kurudi tena Ligi Kuu ikiwa wataifunga Peterborough kwenye Ligi ya Coca Cola Championship na Notingham Forest kufungwa na Bristol City.
Katika Ligi hiyo ya Championship, Newcastle ndio vinara wakiwa na pointi 83 kwa mechi 39, wa pili ni West Bromwich wakiwa na pointi 79 kwa mechi 40 na wa tatu ni Notingham Forest na wana pointi 70 kwa mechi 40.
Kila Timu inatakiwa icheze jumla ya mechi 46 na Timu mbili za juu ndizo zinapanda moja kwa moja kwenda Ligi Kuu.
Timu za nafasi ya 3 hadi ya 6 huandaliwa Mashindano maalum kuipata Timu moja itakayoungana na hizo mbili za juu kuingia Ligi Kuu.

No comments:

Powered By Blogger