Thursday 1 April 2010

Leo ni EUROPA LIGI!
Leo Ulaya, kuanzia saa 4 dakika 5, saa za bongo, kutakuwa na mechi 4 za kwanza za Robo Fainali ya Kombe la EUROPA LIGI na Timu mbili za England, Liverpool na Fulham, bado zipo kwenye mtanange huo. 
Wakati Liverpool yuko ugenini kuivaa Benfica, Fulham yuko nyumbani na atacheza na Wolfsburg.
Mechi nyingine za leo ni Hamburg v Standard Liege na Valencia v Atletico Madrid ikiwa ni mechi ya Timu za Hispania tu.
TATHMINI: 
Benfica v Liverpool
Liverpool leo wapo Estadio da Luz huko Ureno kuchuana na Benfica katika mechi ya kwanza ya Robo Fainali ya EUROPA LIGI na Timu hizi zitarudiana Anfield hapo Aprili 8.
Katika Msimu wa Mwaka 2005/6, Benfica waliibwaga Liverpool nje ya UEFA CHAMPIONS LIGI katika Raundi ya Mtoano ya Timu 16 pale walipoipiga nje na ndani na leo watataka kurudia historia hiyo.
Msimu huu, Benfica iliwatandika Mahasimu wa Liverpool, Everton, katika mechi zote mbili za Makundi ya EUROPA LIGI na Benfica wanaingia kwenye mechi ya leo kwa kujiamini kwa vile wao ndio vinara wa Ligi yao huko Ureno wakiwa mbele kwa pointi 6 dhidi ya Timu inayowafuata.
Kwa Liverpool, EUROPA LIGI ndie mkombozi wao pekee wa Msimu ulioparaganya kwao baada ya kutupwa nje katika kila Kombe na kwenye Ligi Kuu wanachopigania ni, pengine, nafasi ya 4 ambayo hata hiyo haimo mikononi mwao.
Hivyo matokeo mazuri kwa Liverpool katika mechi ya leo ni jambo wanalotaka ili wawe katika nafasi nzuri hapo Aprili 8 watakaporudiana na Benfica huko Anfield.
Katika Kikosi chao, Wachezaji watakaokosekana kwa Liverpool ni Kiungo Alberto Aquilani ambae aliumia enka mazoezini na Maxi Rodriguez ambae haruhusiwi kucheza kwani awali alichezea Klabu nyingine kwenye Mashindano haya.
Wengine ni Martin Skrtel na Fabio Aurelio ambao ni majeruhi wa muda mrefu.
Albert Riera nae ameachwa kabisa kwa matatizo ya nidhamu baada ya kumkashifu Meneja Rafa Benitez.
Nae Staa wa Liverpool, Fernando Torres, ataicheza mechi ya leo kwa tahadhari kubwa kwani anayo Kadi ya Njano na akipewa nyingine leo hataruhusiwa kucheza mechi ya marudiano kati ya Timu hizi mbili.
Nao Benfica watamkosa Mchezaji toka Argentina Javier Saviola ambae ameumia mguu lakini Mfungaji wao bora, Oscar Cardozo, anategemewa kuwepo kilingeni.
Fulham v Wolfsburg
Fulham wapo nyumbani Craven Cottage kucheza na Mabingwa wa Ujerumani na wataombea mwendo wao mzuri kwenye Kombe hili uendelee hasa baada ya kuwabwaga Mabingwa Watetezi wa Kombe hili Shakhtar Donetsk na Vigogo wa Italia Juventus.
Ingawa Woflsburg hawapo timamu msimu huu kwenye Bundesliga na hawategemewa kuutetea vyema Ubingwa wao, Timu hii imeshinda mechi yao ya mwisho huku Fulham wakiwa wametandikwa mechi 3 mfululizo tangu waibwage Juventus bao 4-1.
Fulham watawakosa Nicky Shorey na Stefano Okaka ambao hawaruhusiwi kucheza kwa vile awali walichezea Timu nyingine.
Pia Wachezaji Andrew Johnson na John Paintsil wako nje kwa kuwa ni majeruhi.
Kwa Wolfsburg wasiwasi wao mkubwa ni kama Muuaji wao mkuu Edin Dzeko atakuwa fiti kwani aliumia mazoezini.

No comments:

Powered By Blogger