Burnley 0 Blackburn 1
Leo katika mechi ya Ligi Kuu iliyoanza mapema, Blackburn Rovers wakiwa ugenini Uwanja wa Turf Moor wameitungua Burnley bao 1-0 kwa bao la penalti yenye utata iliyotolewa na Refa Mike Dean kwa madai Kipa wa Burnley Brian Jensen alimwangusha Martin Olsson wa Blackburn.
David Dunn ndie aliefunga bao hilo kwa penalti hiyo kwenye dakika ya 20.
Kipigo hicho kimeifanya Burnley ibaki nafasi ya pili toka mkiani na hivyo kuandamwa na balaa la kuporomoka Daraja.
Ushindi huu unazidi kuwakikishia Blackburn uhai wao kwenye Ligi Kuu.
Mechi ya Ligi Kuu inayofuata baadae leo ni ile mechi ya kumbukumbu ya goli la ‘Bichi Boli’ kati ya Liverpool na Sunderland.
Katika mechi ya kwanza, Sunderland waliifunga Liverpool bao 1-0 lililofungwa na Darren Bent ambae shuti lake liliugonga mpira wa Bichi uliotupwa uwanjani na Shabiki wa Liverpool na kumbabaisha Kipa Reina na kutinga wavuni.
Wenger awaka baada ya droo!
Baada ya jana Timu yake kubanwa na Birmingham na kutoka sare 1-1 Uwanja wa Mtakatifu Andrew, Meneja wa Arsenal Arsene Wenger aliwawakia Waandishi wa Habari waliokuwa wakimhoji baada ya mechi hiyo ya Ligi Kuu hapo jana.
Sare hiyo imewafanya Arsenal warudi nafasi ya 3 wakiwa pointi 4 nyuma ya vinara Manchester United na pointi 3 nyuma ya Timu ya pili Chelsea huku Timu zote zikiwa zimecheza mechi 32 na kubakisha 6.
Wenger alifoka baada ya Waandishi kumuuliza ikiwa anadhani Timu yake inachezewa rafu kusudi, Wenger alijibu kwa hasira: “Mnadhani nadai tunachezewa rafu kusudi? Hebu niacheni! Nikitoa maoni kuhusu mechi nyie mnatafuta utata tu!”
Waandishi hao walitaka kujua maoni ya Wenger baada ya Nahodha wake Cesc Fabregas kuumizwa na Craig Gardner hasa wakikumbuka hiyo ilikuwa ni mechi ya kwanza kwa Arsenal kurudi Uwanja wa Mtakatifu Andrew tangu miaka miwili iliyopita alipoumizwa Mchezaji wao Eduardo alievunjwa mguu na Mchezaji wa Birmingham Martin Taylor.
Katika mechi hiyo, huku Arsenal wakitafuta ushindi ili kujizatiti kuwania Ubingwa, Birmingham walisawazisha dakika za mwisho na kuyavunja matumaini ya Arsenal na hivyo ndivyo ilivyokuwa tena hapo jana wakati Mchezaji alietoka bench Kevin Phillips aliposawazisha kwa Birmingham kwenye dakika ya 92.
Nae Meneja wa Birmingham, Alex McLeish amepinga madai ya kwamba Arsenal wanachezewa rafu kusudi kwa kusema: “Sidhani hilo ni kweli! Hata wao Arsenal wanacheza rafu na ndio maana Refa kawapa Kadi Song na Clichy.”
Fergie asema ilikuwa vita kuwafunga Bolton!
Sir Alex Ferguson amesisitiza Manchester United iko tayari kujibu mapigo yoyote toka kwa Chelsea kufuatia Timu yake kuinyuka Bolton Wanderers bao 4-0 na ushindi huo ulifuata baada ya mapema jana Chelsea kuwafumua Aston Villa 7-1.
Siku ya Jumatano, Chelsea waliichabanga Portsmouth bao 5-0.
Hata hivyo Manchester United ndie anaeongoza Ligi akiwa na pointi 72 na Chelsea wana pointi 71.
Man United na Chelsea watakutana kwenye Ligi wikiendi ijayo Aprili 3 huko Old Trafford.
Kuhusu ushindi wa 4-0 juu ya Bolton waliokuwa wakicheza kwa miguvu na kukamia, Ferguson amesema: “Ilikuwa vita! Haftaimu nilimwambia Refa Martin Atkinson hii ni Soka sio vita! Refa alichezesha vizuri tu! Walitusakama kwa mipira ya juu na Vidic alikuwa na kazi kubwa kuokoa kwa kichwa!”
Hata hivyo katika moja ya mipira hiyo iliyookolewa na Vidic alimuumiza Straika wa Bolton Johan Elmander kwa kiwiko na ikabidi Straika huyo ashonwe nyuzi tano kichwani.
Meneja wa Bolton Owen Coyle amelalamikia kuumia kwa Elmander na kudai ilikuwa ni rafu na anadhani kama Refa angeona angemchukulia hatua Vidic.
Tukio hilo linaweza kumletea matatizo Vidic kwani endapo Refa hataliandika kwenye ripoti yake basi FA inaweza ikalichukulia hatua na kumfanya Vidic aikose mechi ya Jumamosi na Chelsea. Lakini Refa akisema kaliona basi hamna kitu anachoweza kufanywa Vidic.
No comments:
Post a Comment