Friday, 2 April 2010

BIGI MECHI: Manchester United v Chelsea—Refa ni Mike Dean!!!
• Meneja Burnley aita uteuzi wa Dean ni ‘wehu!”
Uteuzi wa Refa Mike Dean kuchezesha lile pambano la Vigogo wa Ligi Kuu, Manchester United v Chelsea, la kesho Jumamosi huko Old Trafford ambalo Wadau wanaamini Mshindi ndie Bingwa, umeitwa ni wehu na Meneja wa Burnley Brian Laws kufuatia uchezeshaji wa Refa huyo wiki iliyopita katika mechi ya Ligi Kuu kati ya Burnley na Blackburn ambapo Mike Dean aliipa Blackburn penalti tata waliyofunga bao lao la ushindi.
Uteuzi wa Refa Mike Dean, ambae ni Refa wa FIFA tangu 2002, umefanywa na Kampuni inayosimamia Marefa wa Kulipwa inayoitwa ‘Professional Game Match Officials Ltd (PGMOL)’.
Mike Dean, miaka 41, mara ya mwisho kuchezesha mechi ya Man United v Chelsea ni Septemba 2007 na alimpa Kadi Nyekundu Jon-Obi Mikel na pia kuwapa Man United penalti dakika za mwisho na Man United walishinda mechi hiyo 2-0 Uwanjani Old Trafford.
Meneja huyo wa Burnley, Brian Laws, amedai Refa Mike Dean alihadaiwa na Mchezaji wa Blackburn Martin Olsson aliejidondosha kusudi akivunga Kipa wa Burnley Brian Jensen alimgusa.
Marudio ya mikanda ya video yalionyesha waziwazi Olsson hakuguswa na Jensen.
Mwenyewe Olsson alikiri baadae “uongo” wake na kusema alifanya hivyo kwa vile wanajua Refa Dean ndie anaongoza kwa kutoa penalti nyingi Ligi Kuu.
Laws amestushwa na uteuzi wa Mike Dean kuchezesha pambano kubwa na muhimu la Man United v Chelsea na amesema: “Ni wehu kumpa Refa huyu mechi hiyo kubwa!”
Laws aliongeza kwa kusema kwa kuwa kumekuwa na malamiko makubwa kuhusu penalti hiyo waliyopewa Blackburn ambayo hawakustahili kuna hatari Dean akaingia kwenye hiyo BIGI MECHI huku akiwa na mawazo ya kutokutoa penalti na hilo huenda likainyimaTimu penalti ya wazi na kweli.
Kutolewa Chelsea UEFA nafuu kwao, Man United na Arsenal waumizwa UEFA!!
Rooney, Fabregas majeruhi!!!!
Huenda Chelsea walipofumuliwa 2-1 na 1-0 na Inter Milan na kubwagwa nje ya UEFA CHAMPIONS LIGI waliona ni balaa kubwa na kuwaacha wenzao Manchester United na Arsenal wakipeta kuingia Robo Fainali ya Mashindano hayo makubwa kwa Klabu huko Ulaya lakini ushiriki wa Manchester United na Arsenal ambako juzi Man United walifungwa 2-1 na Bayern Munich huko Ujerumani na Arsenal kutoka sare 2-2 na Barcelona Uwanjani Emirates, umeleta hasara kubwa na athari kubwa kwa Klabu hizo mbili zinazofukuzana na Chelsea kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu.
Manchester United, ambao kesho Uwanjani kwao Old Trafford wanaivaa Chelsea katika BIGI MECHI ambayo Wadau wanaamini mshindi ndie Bingwa, wataingia Uwanjani bila ya Nyota wao Wayne Rooney alieumia katika mechi na Bayern Munich Jumanne iliyopita.
Arsenal, ambao wapo pointi 4 nyuma ya vinara Man United na pointi 3 nyuma ya Timu ya pili Chelsea, nao walipata pigo kubwa pale Nahodha wao Cesc Fabregas alipovunjika mfupa mmoja wa mguu wake alipogongana na Nahodha wa Barcelona Carles Puyol Timu hizo zilipocheza Jumatano.
Wakati Rooney anategemewa kupona na kurudi Uwanjani ndani ya Wiki 4 na hivyo kuwahi mechi za mwisho za Ligi Kuu inayomalizika Mei 9, Fabregas inaaminika Msimu wake ndio umekwisha na ushiriki wake kwenye Timu ya kwao Spain inayocheza Fainali za Kombe la Dunia litakaloanza Afrika Kusini Juni 11 pia una hatihati.
Mbali ya Fabregas, Arsenal pia waliathirika mno katika mechi hiyo na Barcelona pale William Gallas na Andrey Arshavin kuumia na inasadikiwa wawili hao watakuwa nje kwa kipindi kirefu na huenda Msimu kwao ukawa umekwisha.

No comments:

Powered By Blogger