EUROPA LIGI: Liverpool chali Ureno, Fulham yapeta nyumbani!!
Benfica 2 Liverpool 1
Fulham 2 v Wolfsburg 1
Hamburg 2 v Standard Liege 1
Valencia 2 v Atletico Madrid 2
================================
Benfica 2 Liverpool 1
Penalti mbili zilizopigwa na Oscar Cardozo wa Benfica ndizo zilizoiua Liverpool kwenye mechi ya kwanza ya Robo Fainali ya EUROPA LIGI iliyochezwa Estadio da Luz huko Lisbon, Ureno.
Liverpool walikuwa ndio wa kwanza kupata bao baada ya frikiki ya Steven Gerrard kumaliziwa kifundi na Daniel Agger aliebetua mpira na kufunga hiyo ikiwa dakika ya 9 tu ya mchezo.
Katika dakika ya 30, Liverpool wakajikuta wako mtu 10 pale Babel alipofanya ujinga wa kumsukuma Luisao usoni na Refa Jonas Eriksson kutoka Sweden akamtwanga Babel Kadi Nyekundu.
Babel alikuwa amechukizwa na kitendo cha Luisao kumkata Fernando Fernando Torres kwa nyuma tukio ambalo Refa aliamua ni faulo na kumpa Kadi ya Njano Luisao.
Hadi mapumziko Benfica o Liverpool 1.
Kipindi cha pili Benfica walipata bao la kusawazisha lililioanzia kwa frikiki ya Cardozo nje ya boksi kugonga mwamba na katika kizaazaa golini mwa Liverpool, Beki Insua akamkata Aimar na penalti ikatolewa.
Cardozo akapiga penalti ya chini iliompita Kipa Pepe Reina na kufanya mechi iwe 1-1 katika dakika ya 59.
Kwenye dakika ya 79 krosi ya Di Maria ilimkuta Mlinzi Carragher akiwa mikono mbele na kuucheze mpira huo kwa mkono na Msaidizi wa Refa akamwashiria Refa Eriksson kuwa ni penalti.
Alikuwa Cardozo tena mpigaji wa penalti na alimchambua Kipa Reina kwa mara ya pili na kuandika bao la ushindi kwa Benfica.
Katika mechi ya marudio, Liverpool itamkosa Insua, ambae tayari alikuwa na Kadi ya Njano kabla ya mechi, jana alilambwa tena Kadi ya Njano na hivyo atafungiwa mechi hiyo ya Aprili 8.
Vikosi vilivyoanza:
Benfica: Julio Cesar, Luisao, Pereira, David Luiz, Javi Garcia, Ramires, Aimar, Carlos Martins, Fabio Centrao, Di Maria, Cardozo
Liverpool: Reina, Jonhson, Agger, Carragher, Insua, Gerrard, Mascherano, Lucas,Torres, Kuyt, Babel
Fulham 2 Wolfsburg 1
Fulham wakiwa kwao Craven Cottage walifanikiwa kuifunga Wolfsburg bao 2-1 katika mechi ya kwanza ya Robo Fainali ya EUROPA LIGI.
Mechii hii ilikuwa ngumu na ngome zote zilisimama imara na kufanya nafasi kwa kila upande kuwa nadra sana.
Lakini alikuwa Mshambuliaji anaeng’ara ambae wengi wamepiga mbiu awemo Kikosi cha England cha Kombe la Dunia, Bobby Zamora, alieipatia Fulham bao la kwanza katika dakika ya 59 kwa shuti la kupinda akiwa mita kama 20 nje ya goli.
Dakika 4 baadae, Damien Duff akapachika bao la pili kufuatia Beki wa kushoto Konchesky kupanda juu na kumtilia krosi Zamora alieubembeleza mpira kwenye njia ya Duff aliefunga kwa kujiamini.
Lakini Mabingwa wa Ujerumani, Wolfsburg, wamejipa matumaini pale walipopata goli la ugenini lililofungwa na Madlung dakika ya 89.
Vikosi vilivyoanza:
Fulham: Schwarzer, Hughes, Hangeland, Konchesky, Danny Murphy, Simon Davies, Dickson Etuhu, Bobby Zamora, Damien Duff, Zoltan Gera, Dempsey.
Wolfsburg: Benaglio, Madlung, Barzaqli, Schafer, Pekarik, Josue, Misimovic, Gentner, Edin Dzeko, Grafite
No comments:
Post a Comment