ROBO FAINALI UEFA CHAMPIONS LIGI: Ni leo kindumbwembwe!!!
Bayern Munich v Manchester United
UWANJA: Allianz Arena Saa: 3 dakika 45 usiku [Bongo]
Hili ni pambano ambalo wengi linawakumbusha ile Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI mwaka 1999 ambayo Manchester United wakiwa nyuma bao 1-0 hadi dakika ya 90 walifanikiwa kuiliza Bayern Munich walipopachika bao 2 katika dakika 3 za nyongeza kwa bao za Teddy Sheringham na Ole Gunnar Solksjaer.
Lakini safari hii, hili ni pambano la Robo Fainali na hii ni mechi ya kwanza tu na marudio yake ni Aprili 7 huko Old Trafford nyumbani kwa Manchester United.
Man United wanatinga dimbani wakiwa katika fomu nzuri tu wakiwa wameshinda mechi 8 mfululizo na ya mwisho ikiwa ni ile ya Jumamosi walipoitandika Bolton bao 4-0.
Katika mechi hizo 8 Man United wamefunga jumla ya goli 19 na kufungwa 2 tu huku Rooney akifunga goli 8 na kufanya idadi yake ya magoli msimu huu iwe 33.
Man United wapo kileleni mwa Ligi Kuu.
Bayern Munich, baada ya kuanza Msimu wao kwa kusuasua, waliongeza kasi na nguvu na kuongoza Bundesliga lakini hivi karibuni mambo yameanza kwenda mrama.
Wikiendi hii iliyopita Bayern wameporwa uongozi wao wa Bundesliga na FC Schalke 04 walipotwangwa 2-1 wakiwa uwanja wao nyumbani na Stuttgart.
Kabla ya kipigo hicho, Bayern walipata ushindi mwembamba wa dakika za nyongeza wa bao 1-0 kwenye Kombe la DFB walipoifunga Schalke.
Na kabla ya ushindi huo, katika mechi zao 4 za mwisho, walishinda moja, suluhu moja na kupigwa mbili.
Katika mechi hii na Man United, Bayern huenda wakamkosa Staa wao Arjen Robben alieumia kwenye mechi na Stuttgart.
Lyon v Bordeaux
UWANJA: Stade Gerland Saa: 3 dakika 45 usiku [Bongo]
Hii ni mechi kati ya Klabu za Ufaransa Lyon wakiwa chini ya Kocha Claude Puel na Bordeaux wako chini ya Nahodha wa zamani wa Ufaransa Laurent Blanc ambae aliwahi kuichezea Manchester United.
Wakati Lyon inaingia dimbani ikiwa na Kikosi chake chote bila ya kuwa na majeruhi, Bordeaux watacheza bila Kiungo Alou Diarra ambae amefungiwa baada ya kutolewa kwa Kadi Nyekundu kwenye mechi iliyopita ya UEFA CHAMPIONS LIGI Bordeaux walipoibwaga Olympiakos.
Lyon walinyakua Ubingwa wa Ufaransa mara 7 mfululizo kabla ya kubwagwa na Bordeaux Msimu uliokwisha.
Lyon Msimu huu wamejizolea sifa kubwa walipoitoa Klabu Kubwa,Tajiri na yenye Wachezaji wa bei mbaya kina Ronaldo, Kaka na Benzema, Real Madrid, katika Raundi iliyopita ya UEFA CHAMPIONS LIGI.
Kipa wa Lyon, Hugo Lloris, amejigamba: “Hatushindani na Bordeaux, tunashindana sisi wenyewe! Lazima tuwafunge mechi hii ili tusonge mbele!”
Bordeaux ndio kwanza wametoka kwenye pigo kuu baada ya kufungwa kwenye Fainali ya Kombe la Ligi la Ufaransa na Olympique Marseille bao 3-1 hapo Jumamosi na Meneja Laurent Blanc amenena: “Si rahisi lakini ni bora tunacheza mapema Jumanne na hii ni nafasi kubwa kufuta majonzi yetu!”
Bordeaux msimu huu wameshaifunga Lyon wakiwa kwao Uwanja wao Stade Gerland bao 1-0 mwezi Desemba kwenye mechi ya Ligue 1.
No comments:
Post a Comment