Wednesday 31 March 2010

ROBO FAINALI UEFA CHAMPIONS LIGI: Na leo tena!!!
Arsenal v Barcelona
UWANJA: Emirates Saa: 3 dakika 45 usiku [Bongo]
Hili ni pambano ambalo wengi wanalingojea kwa hamu kubwa hasa kwa vile Timu zote zinasifika kwa kucheza ‘Soka tamu’.
Wakati Arsenal walitoka droo 1-1 na Birmngham kwenye mechi yao ya mwisho ya LIgi Kuu, Barcelona wao wameshinda mechi zao 4 za mwisho za La Liga.
Timu zote hucheza mchezo wa kushambulia na kumiliki mpira na mara nyingi mechi zao huwa na mabao mengi.
Nahodha wa Arsenal, Cesc Fabregas, huenda asicheze mechi hii kwa vile ameumia na kutocheza kwake ni pengo kubwa mno kwa Arsenal.
Hata hivyo Arsenal ina uhakika wa kina Sami Nasri, Andrey Arshavin, Eduardo na Nicklas Bendtner kucheza.
Hata Beki wao wa kutumainiwa, William Gallas, huenda akawa dimbani baada ya kupona na kuanza mazoezi.
Barcelona ni moja ya Timu zinazotegemewa kutwaa Kombe la UEFA CHAMPIONS LIGI hasa kwa vile wao ndio Mabingwa Watetezi.
Barca wanamtegemea sana mmoja wa Wachezaji wanaosifika kuwa ni Bora Duniani-Lionel Messi.
Messi msimu huu amefunga bao 4 kwenye Mashindano haya ya Ulaya na ana jumla ya bao 32 Msimu huu.
Ingawa Messi ndie hatari kubwa ya Barcelona, lakini ukweli ni kuwa bila ya Viungo Andres Iniesta na Xavi, Barca ni Timu ya kawaida tu.
Hata hivyo Iniesta ni majeruhi na huenda asionekane kabisa.
Kwa staili zao za uchezaji, hii ni mechi inayonukia bao nyingi.
Inter Milan v CSKA Moscow
UWANJA: San Siro Saa: 3 dakika 45 usiku [Bongo]
CSKA Moscow wamekuwa na Msimu mzuri kwenye UEFA na wametinga Robo Fainali baada ya kuitandika Sevilla 2-1 huko Spain.
Inter Milan, chini ya Kocha wa zamani wa Chelsea Jose Mourinho, waliipiga Chelsea nje ndani, 2-1 Uwanjani San Siro na 1-0 huko Stamford Bridge, na kujikita Robo Fainali.
Inter Milan wanaingia kwenye mechi hii huku wakiwa wanayumba kidogo kwenye Serie A ingawa bado vinara kwani katika mechi zao 5 za mwisho wameshinda moja, suluhu 2 na wamefungwa 2.
CSKA Moscow ndio kwanza wako freshi kwani Ligi ya Urusi ndio kwanza imeanza tu huku CSKA wakiwa wamecheza mechi 3 tu na kushinda mbili, suluhu 1.
Katika Mashindano haya ya UEFA, Wafungaji wa CSKA ni Milos Krasic na Alan Dzagoev.
Inter Milan wamepata mabao yao kwenye UEFA kupitia Samuel Eto’o, Alberto Diego Milito na Dejan Stankovic.
Ushindi kwa Inter Milan wakiwa kwao San Siro ni muhimu hasa ukizingatia marudio ni Moscow ambako ni pagumu mno kushinda hasa kwa vile mechi inachezwa kwenye uwanja wenye nyasi bandia ambazo ni taabu kuchezea kama hujazizoea.

No comments:

Powered By Blogger