Saturday 3 April 2010

Wenger lawamani!!
• Kuumia kwa Gallas, Fabregas kwamtia matatani!!
Meneja wa Ufaransa, Raymond Domenech, amelaumu uamuzi wa kumchezesha William Gallas kwenye mechi ya UEFA CHAMPIONS LIGI kati ya Arsenal na Barcelona siku ya Jumatano na kusababisha ajitoneshe musuli za mguu ambazo kabla zilimweka nja miezi miwili.
Lakini Meneja wa Klabu ya Gallas, Arsenal, Arsene Wenger, ameutetea uamuzi wa Gallas kucheza mechi hiyo na kusema ulikuwa sahihi kwa vile alipona na kufanya mazoezi siku 10 kabla.
Raymond Domenech, akiongea kwenye Mkutano wa Shirikisho la Soka la Ufaransa, alisema: “Nimeudhika! Ilikuwa mapema mno kumchezesha Mchezaji alietoka kwenye maumivu! Sasa huenda akalikosa Kombe la Dunia!”
Domenech anataka Wachezaji wa Kikosi cha Ufaransa wakusanyike Mei 18 tayari kwenda kambini kwa Fainali za Kombe la Dunia zinazoanza Juni 11 huko Afrika Kusini.
Domenech alikuwepo Uwanjani Emirates Jumatano kushuhudia pambano la Arsenal na Barcelona lakini Wenger alisema: “Sikuongea nae! Nina majukumu na Arsenal. Timu ya Taifa ya Ufaransa ni muhimu lakini kwa Gallas kwanza ni Arsenal kwa sababu wanamlipa mshahara! Wachezaji wakiwa fiti tunawatumia!”
Mbali ya kupata kibano kuhusu uteuzi wake wa Gallas, Wenger pia anaonja joto ya jiwe kwa kumchezesha Nahodha Cesc Fabregas katika mechi na Barcelona huku kukiwa na madai alikuwa na ufa kwenye mfupa wake wa mguu na tatizo hilo likazidishwa kwa kucheza mechi hiyo na sasa yuko nje Msimu wote uliobaki na huenda akalikosa Kombe la Dunia.
Wenger mwenyewe ametoboa kuwa wanafanya uchunguzi wa mkasa wa Fabregas ingawa amedokeza kuwa kabla ya mechi na Barcelona walikuwa na ripoti toka kwa Madaktari wawili tofauti waliochunguza eksirei za Fabregas na kutamka mfupa ulikuwa umechubuka tu na si kuwa na ufa.
Wakati huohuo, Arsenal imethibitisha Andrey Arshavin atakuwa nje kwa wiki mbili akijiuguza musuli ya mguu.
Arshavin alianza mechi na Barcelona lakini ilibidi abadilishwe kipindi cha kwanza baada ya kuumia.
Kwa Wadau wa La LIGA……………………………..
• EL CLASICO ni Aprili 10!!!!
Mechi za wikiendi hii ni za mwisho kwa Vigogo wa Spain, Real Madrid na Barcelona, kabla hawajakumbana hapo Aprili 10 Estadio Bernabeau katika lile pambano murua na tamu linalobatizwa jina la “ El Clasico” na safari hii, El Clasico, ni ngoma ngumu mno hasa kwa vile Timu hizi zinafukuzana na ziko pointi sawa kileleni ingawa Real ndie kinara kwa tofauti ya magoli.
Kila Timu ina pointi 74 na zipo pointi 21 mbele ya Timu ya 3 Valencia huku Timu ya 4 Mallorca ikiwa na pointi 47 tu.
Katika mechi ya kwanza ya La Liga kati ya Timu hizi Msimu huu huko Nou Camp, Barcelona iliibuka mshindi kwa bao la Zlatan Ibrahimovic.
Msimu uliokwisha katika mechi iliyochezwa Bernabeau, Barca waliwafumua Real mabao 6-2.
Wikiendi hii, Barcelona wako kwao Nou Camp kucheza na Athletic Bilbao na Real Madrid wako ugenini kucheza na Racing Santander.
Mbali ya mechi ya La Liga wikiendi hii, Jumanne ijayo ndani ya Nou Campa Barca wanarudiana na Arsenal kwenye mechi ya Robo Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI baada ya kutoka sare 2-2 na Arsenal Jumatano iliyopita huko Emirates.

No comments:

Powered By Blogger