Saturday 3 April 2010

Bila ya Rooney, ushindi upo, adai Fergie!
Wakati akiwahakikishia Waingereza kuwa Rooney hakuumia vibaya, Sir Alex Ferguson pia ameionya Chelsea na Timu nyingine za Ligi Kuu kuwa Manchester United ina uwezo mkubwa wa kushinda bila ya Mfungaji wao huyo bora.
Fergie alisema: “Rooney hakuvunjika mfupa na hakuumia vibaya musuli za enka na hilo ni jambo zuri! Hivyo Taifa liache kusali! Sisi kazi yetu ni kuchagua Timu bila Rooney!”
Ingawa Chelsea wanaona faraja kubwa kupambana na Manchester United Uwanja wa Old Trafford Jumamosi bila Rooney, Fergie amewaonya na kutamka kuwa Timu yake ina uwezo mkubwa wa kushinda mechi hiyo bila ya Rooney.
Fergie amesema: “Nina hakika Wachezaji hawana wasiwasi kumkosa Rooney. Ni pigo kumkosa lakini sisi kuna wakati tuliikosa Defensi yetu yote na tukachechemea na kuongoza Ligi kwa pointi moja!”
Kuhusu Chelsea kutokuwa na mechi wiki nzima wakati wao walicheza Jumanne tena safarini huko Ujerumani, Sir Alex Ferguson amesema hawaoni hilo kama mzigo kwao kwani wao wamezoea kucheza Jumamosi na Jumatano na safari hii wamepata siku 4 kupumzika.
Fergie amesema: “Chelsea wataona ni faida kwao kupumzika wiki nzima. Wakati mwingine inasaidia na wakati mwingine ni hasara kwa vile unaukosa ule mtiririko wa mechi mfululizo na kiwango cha utendaji hushuka.”
Katika mechi ya leo kumekuwa na uvumi mkubwa kuwa Owen Hargreaves ambae amekuwa nje ya uwanja kwa miezi 18, mechi yake ya mwisho ikiwa Stamford Bridge Septemba 2008 Man United walipotoka sare 1-1 na Chelsea, huenda akawepo benchi.
Vikosi vinavyotegemewa kuanza:
Manchester United: Van der Sar, Neville, Vidic, Ferdinand, Evra, Fletcher, Nani, Carrick, Park, Giggs, Berbatov.
Chelsea: Cech, Ferreria, Alex, Terry, Zhirkov, Mikel, Lampard, Malouda, Ballack, Anelka, Drogba.

No comments:

Powered By Blogger