Friday 2 April 2010

Ligi Kuu: Ni uhondo wikiendi hii!
Jumamosi, 3 Aprili 2010 [saa za kibongo]
[saa 8 dak 45 mchana]
Man United v Chelsea
[saa 11 jioni]
Arsenal v Wolves
Bolton v Aston Villa
Portsmouth v Blackburn
Stoke v Hull
Sunderland v Tottenham
[saa 1 na nusu usiku]
Burnley v Man City
________________________________________
Jumapili, 4 Aprili 2010
[saa 11 jioni]
Birmingham v Liverpool
Fulham v Wigan
[saa 12 jioni]
Everton v West Ham
---------------------------------------------------------
Man United v Chelsea
Ingawa hii ni Bigi Mechi lakini kimahesabu siyo itakayoamua nani ni Bingwa ila itaamua nani mwenye nafasi kubwa ya kutwaa huo Ubingwa.
Mechi hii ndiyo ya kwanza kuchezwa kwa wikiendi hii na itaanza saa 8 dakika 45 saa za bongo Uwanjani Old Trafford.
Ushindi kwa Man United, watakaocheza bila Mfungaji wao Bora Wayne Rooney ambae ni majeruhi, utawafanya wawe pointi 4 mbele ya Chelsea.
Mwanzoni mwa msimu, Chelsea waliishinda Man United kwa bao 1-0, bao ambalo lilizua mzozo na mjadala mkubwa kuhusu uhalali wake.
Katika mechi kama hii Msimu uliokwisha, Man United waliikung’uta Chelsea bao 3-0.
Arsenal v Wolves
Baada ya kazi nzito ya Jumatano walipotoka sare 2-2 na Mabingwa wa Ulaya Barcelona kwenye UEFA CHAMPIONS LIGI, Arsenal wapo nyumbani Emirates kucheza na Wolves bila ya Wachezaji wao Cesc Fabregas, Gallas na Arshavin ambao wote waliumia kwenye mechi hiyo na Barcelona.
Wolves wapo kwenye wimbi la kutokufungwa katika mechi 4 na hilo limewafanya wajiwekee tabaka la pointi 5 kati yao na Timu zilizo eneo la kushuka Daraja
Sunderland v Tottenham
Tottenham wapo nafasi ya 4 kwenye Ligi, nafasi ambayo pia inawaniwa na Man City, Liverpool na Aston Villa, na kila mmoja anaitaka nafasi hiyo ili acheze UEFA Msimu ujao.
Lakini wapinzani wa Tottenham, Sunderland, watakuwa nyumbani Uwanja wa Stadium of Light na wao wanapigania kujinusuru kutoshuka Daraja huku Meneja wao Steve Bruce akitaka wajizolee pointi 40 ambazo anahisi ndizo zitawapa usalama.
Sunderland wamebakisha mechi 6 na wapo pointi 5 pungufu ya hizo 40 anazotaka Steve Bruce.
Bolton v Aston Villa
Baada ya kutandikwa na Chelsea 7-1 Jumamosi iliyopita na kukumbwa na uvumi mkubwa kuwa Meneja wao Martin O’Neill anaondoka, Aston Villa wanarudi uwanjani huko Reebok kucheza na Bolton ambayo inapigana kujilimbikizia pointi ili wasivutwe kwenye zile Timu 3 za mkiani ambazo hushuka Daraja.
Stoke City v Hull City
Hull City wanawania ushindi wao wa pili mfululizo baada ya wiki iliyopita kuitungua West Ham lakini Uwanja wa Britannia ni mgumu kupata ushindi.
Msimu huu, Hull hawajahi kushinda mechi mbili mfululizo.
Portsmouth v Blackburn
Portsmouth wako mkiani wakiwa pointi 14 nje ya usalama wa kutoshushwa Daraja na wamebakiza mechi 6.
Kimahesabu, Portsmouth wanaweza kutangazwa wameshuka Daraja wikiendi hii endapo watafungwa na Blackburn na matokeo ya mechi nyingine yakaenda vibaya kwao.
Blackburn wao wameshajihakikishia kubaki Ligi Kuu waliposhinda wiki iliyopita kwa kuifunga Burnley 1-0 na kuzipita pointi 40 ambayo ndiyo Wataalam wanadai ni alama ya usalama.
Burnley v Man City
Wiki iliyopita, Burnley walifungwa hapohapo kwao Turf Moor kwa bao la penalti ya utata mkubwa walipocheza na Blackburn na sasa wanaikaribisha Man City ambao wako kwenye vita ya kuiwania nafasi ya 4.
Birmingham City v Liverpool
Baada ya kupigwa 2-1 na Benfica huko Ureno kwenye EUROPA LIGI, Jumapili Liverpool wanasafiri hadi kwenye Uwanja wa Mtakatifu Andrew kuikwaa Birmingham ambayo ni kigaga wakiwa hapo na hawajafungwa hapo tangu Septemba.
Fulham v Wigan
Fulham waling’ara Alhamisi walipoichapa Wolfsburg 2-1 kwenye EUROPA LIGI na Jumapili wanarudi tena Craven Cottage kucheza na Wigan.
Fulham wako nafasi ya 12 lakini wamefungwa mechi zao 3 za mwisho za Ligi na watataka kubadilisha hali hiyo.
Wigan nao wako chini ingawa si katika zile Timu 3 za mkiani na matokeo mazuri katika mechi zilizosalia zitawapa ahueni zaidi.
Everton v West Ham
Baada ya vipigo 6 mfululizo, uvumi ulizagaa Kocha Gianfranco Zola yuko mguu nje hapo West Ham lakini Zola akauzima uvumi huo na kuipa Timu yake ofu ya siku 3 ili watulize akili.
Everton hawajafungwa katika mechi 5 na wapo nafasi ya 8.

No comments:

Powered By Blogger