Thursday, 30 September 2010

Chelsea wajitayarisha kwa Ze Gunners bila Ancelotti
Chelsea wapo kwenye maandalizi ya BIGI MECHI ya Ligi Kuu ya Jumapili watakapoikaribisha Arsenal Stamford Bridge bila ya Meneja wao Carlo Ancelotti ambae amefiwa na Baba yake mzazi huko kwao Italia.
Giuseppe Ancelotti, Miaka 87, alifariki hapo jana Jumatano na anazikwa Jumamosi.
Carlo Ancelotti yupo huko Italia kwenye msiba lakini Klabu yake Chelsea imethibitisha atakuwepo Stamford Bridge Jumapili kwenye mechi na Arsenal.
Ray Wilkins, ambae ndie Msaidizi wa Ancelotti, ndie anaitayarisha Timu kwa pambano hilo la Jumapili.
Wiki iliyokwisha, Chelsea walipata kipigo chao cha kwanza kwenye Ligi Kuu Msimu huu walipofungwa 1-0 na Manchester City lakini bado wanaongoza Ligi hiyo huku wakiwa pointi 3 mbele ya Manchester United na pointi 4 mbele ya Arsenal.
Wiki iliyopita, Arsenal nao walitandikwa 3-2 na West Bromwich Albion kwenye Ligi.
Ferguson amsifia Hernandez
Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson amemsifia Javier Hernandez, aka Chicharito, baada ya bao lake la dakika ya 85 kuipa ushindi Manchester United wa 1-0 dhidi ya Valencia huko Spain kwenye mechi ya UEFA CHAMPIONS LIGI hapo jana.
Hernandez, maarufu kama Chicharito ikimaanisha njegere ndogo, aliingizwa kipindi cha pili, na Ferguson mwenye furaha alitamka: “Jinsi alivyofunga lile goli ni kama kuchambua njegere! Ana kipaji halisi ingawa inabidi ajenge mwili wake. Ni mmaliziaji mahiri!”
Mwenyewe Chicharito alitamka: “Ni usiku mzuri kwangu. Nina furaha kufunga goli zuri na muhimu. Nlipokuwa nyumbani Mexico tulikuwa tunaangalia UEFA CHAMPIONS LIGI. Ni mashindano makubwa duniani. Ndio kwanza nimeanza kuichezea Man United hivyo kufunga goli UEFA kutanipa imani kubwa. Ni fahari na sifa kubwa kuchezea Man United na nataka hili liendelee muda mrefu.”
Ferguson pia alimsifia Rio Ferdinand ambae jana alicheza dabo Sentahafu na Nemanja Vidic kwa kuleta utulivu kwenye ngome ya Man United ambayo hivi karibuni ilikuwa ikivuja mno.

No comments:

Powered By Blogger