Monday, 27 September 2010

FIFA yamsaidia Kipa wa Togo aliepigwa risasi Angola
Kipa wa Togo Kodjovi Obilale, ambae alijeruhiwa kwa risasi na Waasi wa Cabinda wakati Basi la Timu yao lilipokuwa likiingia Angola toka Congo kwenda kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika na tukio hilo kuwaua Watu wawili kwenye msafara, amesema FIFA imempa msaada wa Dola 25,000.
Obilale, Miaka 25, alipigwa risasi mgongoni na hadi sasa ikiwa Miezi minane imepita hawezi kutembea.
Obilale, aliepokea barua kutoka kwa Rais wa FIFA Sepp Blatter, amesema: “Huu ni wema!”
Kipa huyo wa Togo alikerwa na CAF kwa kutomsaidia na ndipo alipomwandikia barua Sepp Blatter.
Katika barua yake, Blatter ameahidi kulichunguza jalada la Kipa huyo na kumtakia moyo wa kishujaa kukabiliana na matatizo yake.
Obilale alikuwa akichezea Timu ya Daraja la chini huko Ufaransa na hadi sasa hawezi kuusogeza mguu wake wa kulia chini ya goti ambao pia umekufa ganzi.

No comments:

Powered By Blogger