Wednesday 29 September 2010

Mtandao wa Uhamisho Wachezaji wa FIFA rasmi Ijumaa
Kuanzia Ijumaa Wiki hii, Uhamisho wa Kimataifa wa Wachezaji Soka lazima upitie kwenye Mtandao wa Uhamisho wa FIFA ujulikanao kama TMS [Transfer Matching System].
Mwanzoni mwa Mwaka huu wakati FIFA ilipoutambulisha mfumo huo mpya wa Uhamisho ilisema njia hiyo mpya itadhibiti uhamisho wa Kimataifa wa Wachezaji na kuondoa kasoro nyingi zikiwemo zile za Wachezaji kumilikiwa na Kampuni badala ya Klabu wanazochezea na ununuzi wa Wachezaji hao unaohusishwa kuhodhi pesa kinyume cha sheria.
Meneja Mkuu wa TMS, Mark Goddard, alisema: “Mpaka sasa mtindo uliokuwa ukitumiwa ni wa makaratasi kama ilivyokuwa miaka 100 nyuma! Ilikuwa ngumu kufuatilia Wachezaji gani wamehamishwa. Kulikuwa na uhamisho feki, kulikuwa na uuzwaji wa Wachezaji ambao hawapo ili mradi Watu mafisadi wahamishe pesa zao toka Nchi moja hadi nyingine kinyume cha sheria!”
Katika mfumo wa TMS uanaotumia mtandao, ili kukamilisha uhamisho wa Mchezaji inabidi Klabu zinazouza na kununua Mchezaji ziingize kwenye mtandao taarifa zote zinazotakiwa kuhusiana na Mchezaji anaehamishwa zikiwemo ada ya uhamisho, mshahara wa Mchezaji huyo, Wakala wake au Mwanasheria wake na muda wa mkataba wake.
Pia, ada ya uhamisho ni lazima itoke Benki moja kwenda nyingine.
Goddard alisema: “Huu ni mradi mkubwa wa FIFA. Haujabadilisha sheria za uhamisho bali unadhibiti uhamisho na kuondoa kasoro na dosari nyingi.”
Moja ya kasoro hizo ni ile ya Wachezaji kumilikiwa na ‘Watu baki” badala ya Klabu. Mtindo huo ni kitu cha kawaida huko Marekani ya Kusini ambako baadhi ya Wachezaji humilikiwa na Makampuni, Mawakala na hata Mifuko ya Pensheni.
Mfano maarufu ni umiliki wa Mchezaji Carlos Tevez aliechukuliwa na West Ham kutoka Corinthians lakini ikabainika baadae kuwa Corinthians haikuwa ikimmiliki.
West Ham ilipigwa faini ya Pauni Milioni 5.5 Aprili 2007 kwa kukiuka sheria za Ligi Kuu zinazokataza Mchezaji kumilikiwa na Kampuni binafsi badala ya Klabu.
Vilevile, mtindo huu wa TMS utaondoa kesi za madai zinazohusiana na kutolipwa au kutokamilishwa ada ya uhamisho wa Mchezaji kwa vile vitu vyote vitakuwa wazi mtandaoni.
Goddard ameongeza kuwa mtindo huo mpya unarahisisha mno uhamisho wa Mchezaji na akatoa mfano wa Mchezaji mmoja aliehama Klabu moja kutoka England na kwenda Scotland na uhamisho wote ikiwemo kupata kibali cha Kimataifa vilichukua dakika 7 tu na Mchezaji huyo akafanikiwa kuichezea Klabu yake mpya siku hiyo hiyo.

No comments:

Powered By Blogger