Saturday 28 June 2008


MBINU ZA FAINALI: Germany vs Spain
MIFUMO:
Kocha wa Ujerumani Joachim Low itabidi aamue aufuate mfumo upi: ama ule wa 4-5-1 uliowaua vizuri Wareno lakini ulishindwa kufanya kazi vizuri katika mechi na ‘Wapiganaji wa Kituruki’ au fomesheni yake ya kila siku ya 4-4-2.
Nae Kocha wa Spain Luis Aragones yeye ametumia 4-4-2 katika mechi zote za EURO 2008 isipokuwa mechi ya Nusu Fainali dhidi ya Urusi alipolazimika kumtoa pacha mwenza wa Fernando Torres, David Villa alieumia, na kumwingiza staa na kiungo wa Arsenal Cesc Fabregas na hivyo kubadilisha fomesheni na kuwa 4-5-1.
Mfumo huo ulifanikiwa sana na Spain ikaibuka mshindi 3-0 na hivyo watalaam wengi wanahisi ndio utakaotumiwa kwenye fainali.
UBORA:
Ushujaa na moyo thabiti wa kiume wa kutokata tamaa kihistoria ndio nguzo ya Ujerumani. Daima wao wanaamini filimbi ya mwisho ndio inaamua mshindi. Na ndio maana wanaitwa ‘MASHINE YA KIJERUMANI’.
Ubora wa Spain uko kwenye utaalam na ufundi wao wa kusakata kandanda linalodhihirisha vipaji vya hali ya juu. Pamoja na hayo wana mfumo bora wa uchezaji ambao umewafanya wawe hawajafungwa katika jumla ya mechi 21 mpaka sasa.
UDHAIFU:
Germany ilionekana mchovu na ngome yao ilipwaya kwa muda mrefu katika mechi ya Nusu Fainali na Uturuki. Kipa Jens Lehmann, miaka 38, alionyesha kabisa kuwa zama zake zimekwisha na ndio maana ametemwa na Arsenal.
Spain hawana nguvu kwenye mipira ya juu ya vichwa kote kwenye ulinzi na ushambuliaji na hili, ingawa halijawaletea athari kwenye EURO 2008, ndio utakuwa mwanya wa Ujerumani.
NGOME:
Kipa wa Ujerumani na walinzi wanne wa nyuma wana uzoefu mkubwa ingawa walipwaya kwenye mechi ya Uturuki. Walinzi wa kati Per Mertesacker na Christoph Metzelder ni imara kukabili senta fowadi wa aina ya Torress ingawa wanapata shida kuwasimamisha viungo wanaoshambulia wa aina ya Fabregas na Andres Iniesta.
Defensi ya Spain haijapwaya. Kipa Iker Casillas na beki wa kati Carles Puyol bado hawajaifungisha timu huku beki wa kulia Sergio Ramos ameonekana mwepesi sana kupanda juu kwenda kushambulia.
VIUNGO:
Michael Ballack hakung’ara siku alipocheza na Uturuki lakini yeye ni mchezaji mkubwa na ni dhahiri atajituma kwenye mechi hii kubwa ambayo atasaidiwa na viungo wa pembeni mawinga Bastian Schweinsteiger na Lukas Podolski huku Torsten Frings akitegemewa kuongeza moto wa injini ya ‘MASHINE YA KIJERUMANI’.
Pasi zenye uhakika na usahihi za viungo wa Spain pamoja na kuingizwa ‘mpishi’ Fabregas ndicho kilichowaua Warusi. Na kama viungo hao watacheza kama hivyo basi patashika ipo.
MASHAMBULIZI:
Miroslav Klose, ambae amefunga goli moja moja katika mechi zake mbili za mwisho, anaanza kupamba moto kama ule uliomfanya awe Mfungaji Bora katika Kombe la Dunia mwaka 2006. Pia, uwezo wake wa kufunga magoli ya vichwa na udhaifu wa ngome ya Spain kwenye mipira ya juu ndio silaha kubwa ya Ujerumani.
Kumkosa David Villa, ambae ndie anaongoza kufunga magoli EURO 2008, kutamfanya Fernando Torres awe mshambuliaji pekee akisaidiwa na viungo Fabregas na Iniesta.Hata hivyo karata ya trufu ya Spain ni mshambuliaji Daniel Guiza ambae n mfungaji bora wa La Liga huko Spain na ambae bila shaka ataingizwa kipindi cha pili.

No comments:

Powered By Blogger