Saturday 21 June 2008


SAKATA LA RONALDO
-mtaalam achambua kiini!
Cristiano Ronaldo anataka kuhama Manchester United kwa sababu moja tu: klabu hiyo haiwezi kumfanya ashinde TUZO YA MCHEZAJI BORA DUNIANI.
Wakati tangu jana wachezaji wengi wa Man U wamekuwa wakijaribu kumsihi Ronaldo asiondoke kwa kumpigia simu na kumtumia ujumbe wa simu, wengi tunaamini huyo mtoto amekosa fadhila hasa kwa Sir Alex Ferguson mtu ambaye amemlea na kumtetea hasa pale Uingereza nzima ilipomsakama baada ya ‘kusababisha’ Rooney apewe kadi nyekundu kwenye mechi ya Komba la Dunia mwaka 2006.
Sasa imegundulika uchu wa Ronaldo ni kupata Tuzo ya FIFA ya Mchezaji Bora Duniani na bila shaka ameangalia listi ya washindi wa nyuma na akagundua itabidi ahamie Real Madrid ili ashinde tuzo hiyo!
Katika miaka 17 tangu tuzo hiyo ianze kutolewa hakuna hata mchezaji mmoja anaechezea mpira Uingereza aliewahi kushinda! Washindi 9 wa zawadi hiyo wametoka La Liga, ligi ya Uhispania, na wanne kati yao-Luis Figo, Mbrazil Ronaldo, Zinedine Zidane na Fabio Cannavaro-wameshinda wakiwa Real Madrid!
Hicho ndicho kinamfanya Ronaldo akose utiifu na fadhila kwa klabu na watu waliomlea! Manchester United haishindwi kumlipa mshahara ambao Real Madrid wametangaza watamlipa na kuna tetesi watafanya hivyo na hivyo kumfanya yeye awe mchezaji wa soka mwenye mshahara mkubwa katika historia.
Mbali ya Real Madrid kumrubuni, wengi Manchester United wanaamini aliekuwa Meneja wa Ureno ambae sasa anahamia klabu pinzani ya Chelsea Luiz Felipe Scolari ndie mshawishi mkubwa na alitumia muda mwingi kumchota akili Ronaldo ili aione Real kama peponi. Wengi wanahoji nia hasa ya Scolari kama sio kucheza mchezo mchafu wa kuisambaratisha timu pinzani kwako kwa mbinu zilizo nje ya uwanja wa mpira. Ronaldo mwenyewe amekiri Scolari alimshauri ahame.
NINI MAN U WAFANYE?
WAKUBALI UKWELI……………………..
Ronaldo anaondoka na kuwalazimisha Real walipe kitita kikubwa kitakachovunja rekodi ya dunia!
-FAIDA YA UAMUZI HUU: Kitita kitakuwa benki na klabu inaweza kununua lundo la wachezaji!
-HASARA: Watamkosa mchezaji wao bora wa msimu uliopita na pengine watashindwa kung’ara msimu ujao!
MSIMAMO MKALI…………………
Wakatae katakata kuwa Ronaldo hahami na wamshushe Ronaldo achezee timu ya akiba!
FAIDA: Msimamo huu utadhihirisha kwa Real kuwa mchezaji huyo hauzwi.
HASARA: Mchezaji huyo atanuna na kuleta mfarakano kwenye timu hivyo kuvunja morali na umoja.
…………………WAMBEMBELEZE!
Sir Alex Ferguson akae chini na Ronaldo na kumbembeleza abaki kwa kumsihi kuwa mashabiki wa Manchester United wanamtegemea yeye hivyo asiwaangushe na abaki japo msimu mmoja tu!
FAIDA: Man U watakuwa na msimu mmoja mwingine na mchezaji bora duniani ambao utawasaidia Manchester United kupata muda wa kuimarisha kikosi na hivyo hata Ronaldo akihama baadae timu itabaki imara.
HASARA: Dau la Real kumnunua Ronaldo litashuka! Na una uhakika gani Ronaldo hawezi kuumia vibaya?

No comments:

Powered By Blogger