Wednesday, 26 November 2008

LEO KIMBEMBE KWA Chelsea na Liverpool!

Baada ya Mabingwa wa Ulaya Manchester United na Arsenal jana kufuzu kusonga mbele na kuingia Raundi inayofuata ya UEFA Champions League, leo ni zamu ya Klabu nyingine za Uingereza, Chelsea na Liverpool, kucheza na kujihakikishia kusonga mbele.
Liverpool watajihakikishia nafasi ya kusonga mbele endapo watawafunga Marseille ya Ufaransa katika mechi inayochezwa leo usiku nyumbani kwake Anfield.
Lakini Liverpool vilevile anaweza kusonga mbele kwa droo ikiwa Atletico Madrid hatofungwa na PSV Eindhoven katika mechi nyingine ya Kundi lao Kundi D, mechi ambayo itachezwa kwenye Uwanja wa Atletico Madrid uitwao Vicente Calderon ambao Watazamaji leo hawaruhusiwi kuingia kutokana na Atletico Madrid kuadhibiwa na UEFA.
Nao Chelsea, ingawa wanaongoza Kundi A lakini wako kwenye wakati mgumu kufuatia kipigo chao kwenye Kundi hili kwenye mechi yao ya mwisho walipobamizwa 3-1 na AS Roma.
Leo Chelsea wanasafiri hadi Ufaransa kupambana na Bordeaux timu ambayo waliichabanga mabao 4-0 katika mechi yao ya kwanza iliyochezwa Stamford Bridge.
Chelsea atasonga mbele tu endapo atashinda leo. Matokeo yoyote mengine yatawafanya wasote na itawalazimu washinde mechi yao ya mwisho dhidi ya Klabu ya Romania CFR Cluj.
Bordeaux kwa sasa wako pointi moja nyuma ya Chelsea na wamefungana na AS Roma ambao leo wako safarini kuelekea Romania kupambana na CFR Cluj timu ambayo iliwashangaza wengi pale ilipowafunga Roma mabao 2-1 nyumbani kwao!
Mechi nyingine zenye mvuto ni zile za Kundi B ambalo timu zake zote 4 zina nafasi ya kusonga mbele.
Inter Milan, Timu inayoongozwa na Jose Mourinho, Meneja wa zamani wa Chelsea, inaongoza Kundi hili na leo wanahitaji sare tu katika mechi yao dhidi ya Panathinaikos, mechi inayochezwa Milan.
Klabu ya Cyprus, Anorthosis Famagusta, ambayo ilitoka droo ya 3-3 na Inter Milan, inashika nafasi ya pili na itafuzu kusonga mbele endapo leo watawafunga Werder Bremen ya Ujerumani na Panathinaikos wafungwe na Inter Milan.
Katika Kundi C, Barcelona na Sporting Lisbon, wote washafuzu kusonga mbele na kinachogombewa kwa sasa ni nani atakuwa wa kwanza kwenye Kundi hili kitu ambacho kinaweza kuamuliwa leo wakati Sporting Lisbon watakapowakaribisha Barcelona leo usiku.
Mechi nyingine ya Kundi hili ni kati ya Shakhtar Donetsk na Basle ambayo itaamua nani ni mshindi wa tatu na hivyo kucheza UEFA CUP.

No comments:

Powered By Blogger