Sunday, 23 November 2008

Baada ya patashika LIGI KUU jana, wasemavyo Mameneja:

Kufuatia kipigo cha 3-0 mikononi mwa Man City, Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, atamka: 'Ni ushindi unaowakweza Man City. Kisaikolojia timu yangu haikuwa na tatizo kwani tulipigana sana. Tulikosa ukomavu wa kutawala mchezo. Sidhani Man City walitengeneza nafasi nyingi. Nadhani tulitawala mchezo. Hatuna sababu ya kuhamanika ingawa tumefungwa. Tutabadilika!'
Alipobanwa kuhusu utata wa Nahodha wake Gallas alietimuliwa, Wenger alifoka: ' Kwa nini tutoe stetimenti? Tunaweza tukawa na Nahodha na tukambadili bila ya kuvalia njuga suala hilo. Tushawahi kuwa na matatizo. Lakini daima tuna nguvu ya kukabiliana na kila kitu na safari hii tutakabiliana kwa nguvu tena!'

Nae Mark Hughes wa Man City alisema: 'Nadhani ni mara ya pili tunawafunga Arsenal kwenye LIGI KUU kwa hiyo ni ushindi mzuri! Tulikuwa na plani kwa mechi hiyo na tulimudu kuvunja staili yao ya uchezaji. Ila nashangazwa na Wenger kwa kudai hatukustahili ushindi!'

Baada ya suluhu ya 0-0 na Newcastle kwenye ngome yao ya Stamford Bridge, Luis Felipe Scolari, Meneja wa Chelsea amenung'unika: ' Tumecheza asilimia 70 ya mechi upande wao wa kiwanja na kujaribu kufunga mara 10! Wao hawakujaribu chochote! Nani kashinda leo? Ni Newcastle kwani walikuja kutafuta suluhu na wamepata!'
Bosi wa Newcastle, Joe Kinnear, alijibu mapigo: 'Ni mafanikio mazuri na ni mechi tuliyocheza vizuri kupita zote! Kipa wetu Shay Givens alituokoa sana lakini pia kitimu tulifanikiwa. Sidhani Chelsea walitengeneza nafasi yoyote ya wazi ya kufunga! Tumetoka sare na Mabingwa Man U na sasa Chelsea, sidhani mambo ni mabaya!'

Baada ya kuzimwaga pointi mbili nyumbani Anfield, Bosi wa Liverpool, Rafa Benitez, alalama:' Ni siku mbaya, hatukuwa na nguvu na hatukucheza pasi vizuri! Tulipomaliza mechi na kurudi vyumbani, tukagundua Chelsea katoka dro na Arsenal kabamizwa! Matokeo hayo yangekuwa mazuri kwetu kama tungeshinda mechi hii!'

Baada ya mechi za wapinzani wake jana huku akisubiri timu yake Man U ishuke dimbani uwanjani Villa Park kupambana na timu ngumu ya Aston Villa ambayo wiki iliyopita iliikung'uta Arsenal mabao 2-0, Meneja Sir Alex Ferguson alipohojiwa alisema:'Baadhi ya matokeo ya leo yanashangaza lakini si mazuri kwetu endapo tutashindwa kupata pointi 3 leo! Hayo yanafanya mechi hii na Villa kuwa tamu sana!'
Baada ya mechi hiyo ambayo walitoka suluhu ya 0-0 na Aston Villa ambayo wameongeza pengo na Arsenal kuwa pointi 2 na kubaki nyuma ya Chelsea na Liverpool kwa pointi 8 ingawa wana mechi moja mkononi, Sir Alex Ferguson alisema: 'Nadhani tulikuwa timu bora katika mechi yote ukiondoa kipindi cha dakika 15 za kwanza baada ya mapumziko walipotusumbua kwa frikiki na kona. Nimefurahishwa na juhudi zetu dhidi ya timu iliyokuwa ikijihami kutetea maisha yao.'
"

No comments:

Powered By Blogger