Saturday 29 November 2008

MECHI ZA MIAMBA KESHO: Man City v Man U & Chelsea v Arsenal

Tambo na vita ya kisaikolijia vyatawala!!!

Leo kwenye LIGI KUU UINGEREZA kuna mechi 5 zinazochezwa lakini ni uhakika mkubwa kwamba macho ya washabiki wote wa soka la Uingereza pamoja na mioyo yao itakuwa kwenye mechi za kesho za miamba Chelsea watakapowakaribisha Arsenal Stamford Bridge na Manchester City atakapokuwa mwenyeji wa jirani zake wanaoishi maili 8 tu toka City of Manchester Stadium, Mabingwa wa LIGI KUU, Manchester United.
Tayari tambo, majigambo na kauli za kuwaumiza wapinzani kisaikolojia zishaanza kupeperushwa angani.
Wakati juzi nyota wa Man U Wayne Rooney alisema watawaonyesha Man City nani Wafalme wa Manchester, Meneja wa Man U, Sir Alex Ferguson amekaririwa akitamka Man City, mbali ya sasa kutangazwa ni Klabu tajiri duniani hasa baada ya kununuliwa na Koo ya Kifalme ya Abu Dhabi ambayo ni sehemu ya nchi tajiri sana duniani, Falme ya Nchi za Kiaarabu, si tishio na si lolote wala chochote na ndio maana wako nafasi ya 11 kwenye ligi.
Hata hivyo Sir Alex Ferguson amemsifia staa wa Man City Mbrazil Robinho ambae amesema ana kipaji cha hali ya juu.
Man U wanategemewa kumkaribisha tena Mshambuliaji Dimitar Berbatov aliekosa mechi mbili kwa kuwa na maumivu.
Mark Hughes, Meneja wa Man City, ambae aliwahi kuwa mchezaji chini ya Sir Alex Ferguson, amekiri mechi itakuwa ngumu kwani Man U ni timu bora.
Nae Meneja wa Chelsea Luis Felipe Scolari hakuikandya Arsenal na badala yake amesema hata Arsenal inaweza kuwa bingwa mbali ya kuwa pointi 10 nyuma ya wao Chelsea wanaoongoza ligi.
Scolari amedai bingwa wa ligi anapatika mwisho wa ligi na si sasa.
Bosi wa Arsenal Arsene Wenger ambae timu yake haina mwendo mzuri kwenye ligi amekaririwa akisema: 'Watu wameshatufuta kwenye ligi hii. Ni kweli huwezi kusema utachukua ubingwa wakati uko pointi 10 nyuma lakini unaweza kusema njia pekee ya kurudi kwenye kinyang'anyiro ni kuamini unaweza kuwa bingwa! Ndio maana tutaingia kwenye mechi Jumapili tukijiamini tunaweza kuwafunga! Hicho ni kitu pekee unataka wachezaji wako wafanye.'

Katika mechi hiyo Arsenal watapata nguvu kidogo hasa baada ya mastaa wao majeruhi Adebayor, Sagna na Samir Nasri kupona huku Chelsea watamkosa Mshambuliaji Didier Drogba alie kifungoni kwa mechi 3 pamoja na Beki Ricardo Carvalho, Essien na Belletti walio majeruhi.

No comments:

Powered By Blogger