Saturday 29 November 2008

ARSENAL WATHIBITISHA 'VIJISENTI' VYA KUNUNUA WACHEZAJI VIPO!!!!

Mwenyekiti wa Klabu ya Arsenal Peter Hill-Wood aliezuka hivi juzi kumtetea Meneja wake Arsenal amethibitisha Meneja huyo atapewa pesa ili kununua Wachezaji awatakao pindi dirisha la uhamisho litakapofunguka mwezi Januari.
Arsenal kwa sasa wako nafasi ya 5 kwenye msimamo wa ligi wakiwa nyuma ya vinara Chelsea, Liverpool, Manchester United na Aston Villa huku wakiwa nyuma ya Chelsea, timu ambayo wanacheza nayo kesho Jumapili, kwa pointi 10.
Wenger huwa anapenda kutafuta na kukuza chipukizi na ni nadra sana ananunua Wachezaji wa bei mbaya lakini Klabu hiyo haijatwaa Kombe lolote lile tangu 2005 na mashabiki wameshaanza shinikizo kwake ili aingie sokoni kutafuta Wachezaji bora.
Mwenyekiti Hill-Wood aliiambia Arsenal TV: 'Wenger atapewa pesa za kununua Wachezaji. Yeye ni mtulivu katika kununua Wachezaji na hawezi kununua tu ili mradi mashabiki au magazeti yanataka!'
Mwishoni mwa msimu uliokwisha Arsenal iliwapoteza Wachezaji Mathieu Flamini, Alexander Hleb, Gilberto Silva na Philippe Senderos (kwa mkopo) waliohama na Samir Nasri, Aaron Ramsey, Amaury Bischoff na Mikael Silvestre wakanunuliwa.

NEWCASTLE WAMWONGEZA MKATABA MENEJA JOE KINNEAR!!

Joe Kinnear amesaini mkataba wa kuendelea kuwa Meneja wa Newcastle hadi mwisho wa msimu huu.
Kinnear alitua Newcastle mwezi Septemba baada ya Kevin Keagan kubwaga manyanga na aliwekwa hapo kama mtu wa muda tu kwa mkataba wa mwezi hadi mwezi hadi klabu itakapouzwa lakini kumekuwa na ugumu mkubwa kupata mnunuzi.
Kabla ya kuja Newcastle, Joe Kinnear, alikuwa akifundisha Nottingham Forest hadi 2004 na tangu wakati huo mpaka Septemba 2008 alipotua Newcastle alikuwa hana kibarua chochote.

WINGA ZORAN TOSIC KUTUA MAN U JANUARI!!

Mabingwa wa Uingereza na Ulaya, Manchester United, wamefanikiwa kupata kibali cha kufanya kazi kwa Winga chipukizi wa Kimataifa wa Serbia Zoran Tosic [21] ambae ilibidi aombewe kibali hicho kwa sababu alikuwa hajacheza asilimia 70 ya mechi zilizochezwa na Timu ya Taifa ya Serbia za hivi karibuni.
Meneja wa Man U, Sir Alex Ferguson, aliongoza jopo la maofisa wengine wa Mabingwa hao kwenda kutoa utetezi kwenye Tume inayotoa vibali vya kazi mjini Sheffield na sasa Winga huyo anaechezea Klabu ya Serbia Patizan Belgrade yuko huru kujiunga na Man U ifikapo Januari wakati dirisha la uhamisho litakapofunguka.
Zoran Tosic, aliechezea Timu ya Taifa ya Serbia mara 12, atakuwa Mserbia wa pili kwenye timu ya Man U, mwingine akiwa Beki mahiri Nemanja Vidic.

No comments:

Powered By Blogger