Monday 24 November 2008

Wenger amtetea Gallas!

Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, amesimama kidete na kumtetea William Gallas, Mchezaji aliemvua madaraka ya Ukepteni wa timu hiyo, kwa kusema: 'Sijuti kumchagua Nahodha. Yeye aliyaweka matatizo yote ya timu moyoni mwake! Alifanya kazi ya Unahodha kwenye mazingira magumu ya kuandamwa na mapaparazi. Inafika hatua hatutaki presha ihujumu timu!'
Arsenal imemteua kijana Cesc Fabregas [21] kuwa Nahodha mpya wa timu [pichani kulia Fabregas na Gallas wakiwa mazoezini leo].
Wenger vilevile alikanusha madai ya magazeti kuwa dirisha la uhamisho likifunguliwa Januari basi Gallas atauzwa kwa kutamka: 'Ni maoni yao, siwezi kuyazuia. Namheshimu sana William kama mtu na mchezaji na uhusiano wetu hauyumbi kwa haya! Kwangu, yeye ni mchezaji thabiti kwa klabu. Hii inaweza kuwa mwanzo mpya kwake na kumfanya awe mchezaji bora zaidi!'
Wenger akaongeza: 'Kepteni ni sauti ya klabu nje. Lakini yeye ni mmoja tu wa viongozi ndani ya chumba cha kubadilisha jezi wachezaji. Siamini hata chembe Nahodha pekee ndio mtu pekee wa kuongoza Wachezaji!'
Wenger alimalizia kwa kugusia Arsenal inavyoyumba uwanjani: 'Kwa Waandishi Habari, kila kitu ni ama balaa au bora! Hawajui ukweli huwa katikati! Si kila kitu ni kiama na mateso tu! Hii ni nafasi nzuri kwetu kuonyesha tunaijali, kuipenda klabu na kudhihirisha uwezo wetu!'

No comments:

Powered By Blogger