Thursday 27 November 2008

Rooney awabeza Man City: 'SISI NDIO WAFALME WA MANCHESTER'

Wayne Rooney wa Manchester United [pichani kushoto] amewasha utambi kwa kuwabeza wapinzani wao wa jadi Manchester City kabla ya patashika yao ya Jumapili itakayochezwa City of Manchester Stadium nyumbani kwa Man City.
Rooney ametamba: 'Tutawaonyesha kwamba sisi ni Wafalme wa Manchester!'
Msimu uliokwisha Rooney hakucheza mechi zote mbili timu hizi zilipopambana kwani ya kwanza alikuwa kavunjika kidole na ya pili alikuwa kafungiwa mechi moja.
Mechi zote hizo mbili ziliisha kwa ushindi wa Man City.
Mpaka sasa msimu huu, Man U ambae ni Bingwa mtetezi wa LIGI KUU yuko nafasi ya 3 huku Man City akiwa wa 11 na akiwa pointi 4 tu juu ya timu 3 za mwisho kwenye msimamo wa ligi.
Man City hivi karibuni wamenunuliwa na Koo ya Kifalme kutoka Abu Dhabi ambayo ni sehemu ya Falme ya Nchi za Kiarabu, nchi ambayo ni moja ya nchi tajiri sana duniani, na matajiri hao walionyesha kucha zao pale walipomnyakua staa wa Brazil Robinho [pichani kulia] toka Klabu kiburi ya Real Madrid dakika za mwisho kabla dirisha la usajili halijafungwa mwishoni mwa mwezi Agosti kwa uhamisho wa Pauni milioni 32.5 ambayo ni rekodi kwa Uingereza.
Ingawa Man City wana staa Robinho akisaidiwa na Wabrazil wengine Jo na Elano ambao wote wapo Timu ya Taifa ya Brazil, mwendo wao kwenye LIGI KUU ni wa kusuasua na wa kutoridhisha ingawa mechi yao ya mwisho walicharuka pale walipoinyuka Arsenal mabao 3-0.

No comments:

Powered By Blogger