KOMBE LA MABARA: Nini Tathmini ya FIFA kwa Afrika Kusini kuandaa KOMBE LA DUNIA mwakani?
Kombe la Mabara lilishindaniwa na Timu 8 tu, Brazil ikaibuka kidedea, mechi kuchezwa kwenye Miji minne tu na wengi wa Watazamaji kuwa ni Raia wa Afrika Kusini.
Mwakani, kwenye Fainali za Kombe la Dunia, hali itakuwa tofauti kabisa kwani Washabiki Wageni zaidi ya 500,000 watatua Afrika Kusini kuziona Timu 32 zikicheza mechi kwenye Viwanja 10 kila kona ya Afrika Kusini.
Hata hivyo kuandaa na kuendesha Kombe la Mabara kumewapa Afrika Kusini nafasi nzuri kujifunza nini wategemee mwakani na vilevile kuwapa fursa FIFA kutoa tathmini na pia kuangalia wapi pana mapungufu.
FIFA, wakilinganisha mahudhurio ya mechi za Kombe la Mabara yaliyopita, wameridhishwa kuwa mahudhurio yalikuwa bora kwani, kulingana na Danny Jordaan, Mwandalizi wa Fainali za Kombe la Dunia 2010, wastani wa Washabiki 38,000 walitizama mechi wakati huko Ujerumani mwaka 2005 lilipochezwa Kombe la Mabara ni wastani wa Washabiki 37,000 tu walihudhuria.
Huko Ufaransa mwaka 1997 ni watu 30,000 tu waliona mechi uwanjani.
Hata hivyo, mapengo mengi yalionekana Uwanjani wakati wa mechi na hata zile za Nusu Fainali kati ya Bafana Bafana na Brazil na pia Fainali ya jana mechi zote zikiwa Uwanja wa Ellis Park, Johannesburg.
Tathmini inasema hiyo imetokana na sababu kadhaa zikiwemo Tiketi kuuzwa mara 3 zaidi ya bei ya zile mechi za Ligi Kuu ya Bondeni na pia mechi kama ile kati ya Iraq na New Zealand kutokuwa na mvuto kwa Mashabiki.
Sababu nyingine ni kuwa wakati huu ni msimu wa baridi huko Afrika Kusini na Mashabiki wamezoea mechi zao kuchezwa majira ya joto.
Lakini, FIFA imesema kuna maombi ya tiketi zaidi ya 500,000 kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia na Asilimia 80 ni ya Raia wa Kigeni.
Kitu kingine kilichozua mjadala ni VUVUZELA.
Katika kila mechi sauti kubwa za tarumbeta za plastiki, mithili ya kundi kubwa la Tembo wakivamia, zilitawala.
Blatter, pamoja na Timu nyingi za Kigeni, walionyeshwa kukerwa na kelele hizo lakini Danny Jordaan anasema: ‘Ni kweli Vuvuzela lina mikelele lakini kwenye Kombe la Dunia kwenye mechi za Brazil au England kutakuwa na Vuvuzela chache kwani Mashabiki wa Nchi hizo watajazana!’
Kombe la Mabara lilichezwa kwenye Viwanja vinne-Ellis Park, Johannesburg, Free State, Bloemfontein, Royal Bafokeng, Rustenburg na Loftus Versfeld, Pretoria-vyote vikiwa pia ndivyo vitakavyochezewa Fainali za Kombe la Dunia pamoja na Viwanja vingine 6 vipya vinavyojengwa kikiwemo kile kikubwa kupita vyote ambazo mechi za ufunguzi na Fainali zitafanyika, Kiwanja chenye uwezo wa kuchukua Washabiki 94,000 kiitwacho Soccer City huko Soweto, Johannesburg.
Soccer City kitakamilika Desemba na kukabidhiwa kwa FIFA Machi mwakani.
Soccer City kimejengwa kwenye saiti iliyokuwa Uwanja wa FNB, uwanja ambao Nelson Mandela alitoa hotuba yake ya kwanza mara baada ya kutoka jela mwaka 1990.
Tatizo kubwa lililojitokeza wakati wa Mashindano ya Kombe la Mabara na FIFA kuliona ni uhaba wa maeneo ya kupaki magari kwenye Viwanja vingi ukiondoa kile cha Soccer City chenye eneo la kuegesha magari 15,000.
Usafiri wa kwenda na kutoka Viwanjani kwa kutumia Mabasi umekuwa hamna na Mashabiki imebidi watembee kwa miguu, waendeshe gari zao au wakodi teksi.
Lakini Mji wa Johannesburg, ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, unaanzisha Usafiri maalum wa Mabasi yaendayo Kasi, mradi ambao umepingwa vikali na wenye teksi.
Juu ya yote, tatizo kubwa kwa wengi ni hali ya usalama na uhalifu uliokithiri huko Bondeni.
Kwenye Kombe la Mabara hili liliibuka vibaya pale Timu za Misri na Brazil kuibiwa Hotelini mwao.
Hata hivyo Danny Jordaan amesisitiza Serikali ya Afrika Kusini inalipa kipau mbele tatizo hilo sugu na imewekeza zaidi Rand Bilioni 1.3 kulikabili.
Mbali ya mikakati ya maandalizi ya Kombe la Dunia mwakani, kwa wengi na hasa Danny Jordaan, mchezo wa kuridhisha wa Bafana Bafana umewatia moyo washabiki wengi hasa mechi dhidi ya Brazil na ile ya kutafuta Mshindi wa 3 na Spain.
Danny Jordaan anasema: ‘Tuna Mashabiki zaidi ya Milioni 2 hapa Nchini ambao ni Wazungu na hushabikia Manchester United, Liverpool na Chelsea lakini kwenye Kombe hili la Mabara wote walikuwa Bafana Bafana!’
Jordaan anakiri kuwa ili Kombe la Dunia liende vizuri ni lazima nayo Bafana Bafana ifanye vizuri.
Juu ya yote, Jordaan anakubali tatizo la Ulinzi na Usafiri ndilo kubwa kupita yote ingawa kwa ujumla anakubali Kombe la Mabara lilifanikiwa.
No comments:
Post a Comment