Friday, 3 July 2009

Michael Owen asaini mkataba wa miaka miwili Man U!!!
Mshambuliaji wa England, Michael Owen, miaka 29, ambae mkataba wake Klabuni Newcastle ulimalizika Julai 1, leo amesaini mkataba wa miaka miwili na Mabingwa wa England, Manchester United.
Sir Alex Ferguson ametamka: ‘Owen ni Mchezaji wa kiwango cha juu sana duniani na ni mfungaji mahiri na hilo huwezi kulibishia! Ujio wake Manchester United na matumaini ambayo tunayo yatampa changamoto!’
Michael Owen mwenyewe amesema: ‘Nilikuwa nimeanza majadiliano na baadhi ya Klabu za Ligi Kuu lakini, bila kutegemea, Sir Alex akanipigia simu Jumatano mchana na kunialika kifungua kinywa siku ya pili ndipo siku hiyo akaniambia anataka nijiunge Manchester United! Sikusita hata sekunde moja! Nikakubali hapohapo!’ Hii ni nafasi bora sana kwangu na nimeipokea kwa mikono miwili!’
Owen akaongeza: ‘Nategemea kwa hamu kubwa sana kuanza mazoezi na Timu hii Wachezaji wakirudi likizo na nna bahati kubwa nawajua Wachezaji wengi hapa! Napenda nitoe shukrani zangu za dhati kwa Sir Alex Ferguson kwa imani yake kwangu na ninamhakikishia nitalipa fadhila yake kwa magoli na uchezaji wangu!’
Wadau wengi wanaamini kwa Sir Alex Ferguson kumsajili Michael Owen ni kucheza tombola kwa vile miaka ya hivi karibuni ameandamwa na kuumia mara kwa mara lakini pia inaweza ikawa ni karata ya trufu kama aliyoicheza wakati ule alipowasaini Henrik Larson na Teddy Sheringham, Wachezaji ambao wengi waliamini wamekwisha na ilikuwa makosa kwa Sir Alex Ferguson kuwachukua, lakini baadae, watu wote, baada ya Wachezaji hao kung’ara, wakakubali kuwa Ferguson ni mchawi na alifanya sahihi kuwasajili Larson na Sheringham.

No comments:

Powered By Blogger