Monday 29 June 2009

LEO FAINALI ULAYA YA VIJANA CHINI YA MIAKA 21: England v Germany
UWANJA: NEW STADIUM, Malmo, Sweden SAA: 3.45 usiku [bongo]
Timu ya Taifa ya England ya Vijana Chini ya Miaka 21 leo inakutana Fainali na wenzao wa Ujerumani huko Malmo, Sweden kugombea Ubingwa wa Ulaya.
Hii itakuwa mara ya pili kwa Timu hizi kukutana kwenye Fainali za Kombe hili huko Sweden kwani walikuwa Kundi moja mechi za awali na kutoka suluhu 1-1.
Kwenye Nusu Fainali, England iliwabwaga Wenyeji Sweden kwa matuta baada ya dakika 120 kwisha kwa Timu kuwa sare bao 3-3.

Katika mechi hiyo, England walikuwa wakiongoza 3-0 hadi mapumziko lakini Sweden walisawazisha kipindi cha pili.
Ujerumani wametinga Fainali baada ya kuifunga Italia bao 1-0.
England inaongozwa na Meneja Stuart Pearce ambae ni Mchezaji wa zamani England aliewahi kuwa Meneja wa Manchester City na itabidi leo afanye mabadiliko kwa kuwakosa Kipa wake wa kwanza Joe Hart, Washambuliaji Frazier Campbel na Gabriel Agbonlahor ambao wote wanaikosa Fainali kwa kuwa na Kadi.
Leo England itawategemea sana Nyota Chipukizi wa Arsenal, Theo Walcott, Viungo Fabrice Muamba, Mark Noble na Lee Cattermole huku Ngome ikisimamiwa na Nedum Onuoha na Micah Richards wa Manchester City pamoja na Beki wa kushoto wa Arsenal, Kieran Gibbs.
Nao Wajerumani chini ya Meneja Horst Hrubesch wana imani wataimudu England huku Meneja huyo akitamka: ‘Ile mechi ya Makundi, England walituzidi kidogo lakini safari hii hilo halipo.’
Ujerumani walitoka suluhu 0-0 na Spain, kuwafunga Finland 2-0, sare na England 1-1 kwenye mechi za awali za Kundi lao na Nusu Fainali kuibwaga Italia 1-0.
Mchezaji wa Ujerumani Ashkan Dejagah haruhusiwi kucheza Fainali kwa kuwa na Kadi na nafasi yake itachukuliwa na Sandro Wagner.
Rooney: ‘Nitabeba mzigo wote!’
Wayne Rooney amewahakikishia Mashabiki wa Mabingwa Manchester United kwamba anaweza kuchukua nafasi na kuziba mapengo ya Ronaldo na Tevez.
Manchester United imewapoteza Cristiano Ronaldo anaehamia Real Madrid na Carlos Tevez ambae nae pia anaondoka baada ya kuikataa ofa ya Man U lakini Rooney, licha ya kuamini kuwa Meneja wake Sir Alex Ferguson atanunua Wachezaji na kuimarisha Kikosi, amedai kuwa ana uwezo wa kufunga magoli kama walivyokuwa wakifanya Ronaldo na Tevez.
Rooney amesema: ‘Cristiano na Tevez walitufungia magoli mengi sana msimu uliokwisha na ule uliopita nyuma yake lakini nina uwezo wa kuziba pengo hilo. Nilishasema kabla kwamba nikipangwa nafasi nzuri nina uwezo wa kufunga! Wengi wanajua nikicheza kama Sentafowadi nakuwa bora!’
Msimu uliokwisha, mara nyingi Rooney alikuwa akipangwa pembeni na mara nyingine nyuma ya Mshambuliaji mkuu.

No comments:

Powered By Blogger