Tuesday 30 June 2009

Tevez amlaumu Fergie!!!!
Carlos Tevez hakucheza Fainali ya Roma kati ya Barcelona na Manchester United, mechi ambayo Man U walifungwa 2-0 na badala yake Sir Alex Ferguson akaanza na Kikosi chenye Washambuliaji Ronaldo,Park Ji-sung na Wayne Rooney, na sasa Tevez anadai kuwekwa kwake benchi ni makosa na ndio kumesababisha Man U kufungwa.
Tevez, ambae ameikataa ofa ya Man U na sasa yuko mbioni kwenda Klabu nyingine baada ya mkataba wake wa kuwa hapo Old Trafford kumalizika leo, amelalama: ‘Huwezi kumbishia Alex Ferguson! Yeye ni kama Rais wa England! Siku zote huwezi kumshinda kwani utashindwa tu! Lakini alifanya kosa kuniweka benchi! Hiyo ndio fainali pekee Man U wameipoteza tangu niwe hapo!’
Wakala wa Eto’o adai hang’oki Barca ng’oo!!
Josep Maria Mesalles, Wakala wa Mshambuliaji kutoka Cameroun Samuel Eto’o anaechezea Barcelona, aliitisha mkutano wa Waandishi Habari ili kuvunja utata kuhusu Mteja wake ambae mkataba wake na Barcelona unamalizika mwishoni mwa msimu ujao na kutamka kuwa Eto’o ameongezewa miaka miwili na Barca kwa vipengele vilevile vilivyomo kwenye mkataba wa sasa.
Wakala huyo amelazimika kusimama kidete huku kukiwa kumezagaa taarifa kuwa Manchester City imetoa ofa ya Pauni Milioni 25 kumnunua Eto’o na kumpa mkataba ambao masilahi yake ni makubwa mno kiasi ambacho Rais wa Barca Joan Laporta kuuita ni mkataba wa ‘hali ya juu mno!’
Hata hivyo Wakala Josep Maria Mesalles hakufunga milango na ametamka: ‘Eto’o anarudi mazoezini Julai 20 kutoka mapumziko. Kama kuna ofa kutoka Man City yenye uzito na Barca wameiafiki basi na sisi hatuoni ugumu kufikia makubaliano.’

No comments:

Powered By Blogger