Tuesday, 30 June 2009

NI RASMI, VALENCIA YUKO OLD TRAFFORD!!
Manchester United, kupitia tovuti yake, imethibitisha imefanya usajili wake wa kwanza kwa ajili ya msimu ujao baada ya kumnunua Winga kutoka Ecuador, Antonio Valencia, aliekuwa akichezea Timu ya Wigan kwa mkataba wa miaka minne na dau ambalo halikutajwa.
Valencia, umri miaka 23, ameshaichezea Nchi yake mara 34 na kufunga mabao manne.
Sir Alex Ferguson ametamka mbele ya Valencia waliposaini mkataba: ‘Antonio ni Mchezaji tuliekuwa tukimhusudu kwa muda sasa na baada ya kuwa Ligi Kuu kwa miaka miwili sasa nina uhakika kasi yake na kipaji chake itasaidia sana Kikosi chetu.’
Valencia nae alizungumza: ‘Kujiunga Manchester United ni ndoto iliyotimia kwangu! Nilifurahi nilipokuwa Wigan lakini sasa nna nafasi ya kupata mafanikio makubwa hapa! Kucheza mbele ya Washabiki 76,000 na kucheza pamoja na kina Rooney, Ferdinand na Giggs ni kitu cha kustaajabisha kwangu! Siwezi kujizuia kwa hamu yangu!’
Blackburn yamnasa Chipukizi toka Ufaransa N’Zonzi!!
Blackburn Rovers, chini ya Meneja Sam Allardyce, leo wamefanya usajili wao wa nne kwa msimu ujao baada ya kumnasa Kiungo wa miaka 20 kutoka Ufaransa aitwae Steven N’Zonzi aliekuwa akichezea Klabu ya Amiens ambayo imeshushwa Daraja huko Ufaransa.
Blackburn pia imewasaini Walinzi Gael Givet na Lars Jacobsen na Kiungo kutoka Bondeni Elrio van Heerden.
Bosi Sam Allardyce ameonyesha nia yake kumsaini Mchezaji wa tano ambae ni Mkongwe wa Real Madrid Ruud van Nistelrooy.
Maldini agoma kufundisha Chelsea!!
Meneja wa Chelsea, Mtaliana Carlo Ancelotti, amekiri kuwa ofa yake kwa Paolo Maldini ajiunge nae Stamford Bridge ili kuwa mmoja wa Makocha imetupwa chini na Maldini ambae alistaafu kucheza soka AC Milan msimu ulioisha mwezi Mei ambako walikuwa pamoja na Ancelotti.
Ancelotti anasema: ‘Nilimpa ofa lakini amekataa kwani anataka mapumziko toka kwenye Soka.’
Tangu itangazwe Carlo Ancelotti kuwa Meneja mpya hapo Chelsea Klabu hiyo haijasaini Mchezaji yeyote mpya kwa msimu ujao na Ancelotti anasema: ‘Soko la Uhamisho limekuwa gumu! Baada ya Ronaldo kuhamia Real, kila kitu kimepata wazimu!’
Mmisri Zaki anataka kurudi Wigan
Amr Zaki anataka kurudi Klabu ya Wigan Athletic na ana matumaini Meneja mpya wa Klabu hiyo Roberto Martinez atampa mkataba wa kudumu.
Zaki alikuwa Wigan msimu uliokwisha kwa mkopo kutoka Zamalek ya Misri lakini akajiingiza matatani na aliekuwa Meneja wa Wigan Steve Bruce baada ya kuwa na tabia ya uchelewaji kurudi Klabuni kila anapoenda kwao MIsri kuichezea Nchi yake kwenye mechi za Kimataifa hali iliyomfanya Steve Bruce agome kumchukua kwa mkataba wa kudumu ingawa aling’ara Wigan.
Baada kuhama Steve Bruce kwenda Sunderland na ujio wa Meneja mpya Roberto Martinez kumpa matumaini mapya kurudi Wigan, Zaki anasema: ‘Nataka kubaki Wigan. Nasikia Martinez ni Kocha mwenye kipaji na bado Kijana na hivyo yuko karibu na Wachezaji.’

No comments:

Powered By Blogger